Tuesday, December 10, 2013

Nelson Mandela
MARAIS 91 akiwemo Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta ni miongoni mwa viongozi wengine kutoka pembe zote ulimwenguni wanaotarajiwa kuhudhuria ibada ya wafu ya aliyekuwa Rais wa Afrika Kusini, Nelson Mandela, Jumanne mjini Johannesburg.

Huo unatarajiwa kuwa mkusanyiko mkubwa zaidi kuwahi kushuhudiwa katika karne hii, ambapo marais wanne wa Amerika watahudhuria. Itakuwa pia mara ya kwanza kwa  marais wanne wa Amerika katika kipindi cha miaka 15 kuhudhuria hafla ya
aina hiyo kwa pamoja.

Rais Kenyatta aliondoka Kenya mwendo wa saa kumi na mbili jioni Jumatatu kuelekea Afrika Kusini. Kwa mujibu wa Chumba cha Habari cha Rais (PSCU), Rais Kenyatta aliyeandamana na mkewe Margaret aliagwa uwanja wa ndege na Naibu Rais William Ruto.

Mandela ameombolezwa ulimwenguni kote katika makanisa, misikiti na masinagogi na kupelekea maombolezo yake kuwa ya kipekee kuwahi kuunganisha makabila na dini zote ulimwenguni.

Maombolezo yake yanaweza kulinganishwa na ya aliyekuwa Rais wa Amerika J F Kennedy, aliyeuawa mnamo 1963, na yale ya Binti Mfalme Diana aliyefariki kwenye ajali ya barabarani mnamo Agosti 31, 1997. Mengine ni ya Papa John Paul wa Pili aliyefariki mnamo 2004 na kuombolezwa ulimwenguni kote.

Mazishi ya Mandela yatahudhuriwa na Rais Barack Obama na mkewe Michelle, waliokuwa marais George Bush, Bill Clinton na Jimmy Carter. Rais Obama, mkewe Michelle na aliyekuwa Rais George Bush na mkewe Laura waliondoka Jumanne Amerika kuelekea Afrika Kusini.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN) Ban Ki-Moon pia atahudhuria.

Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu hatahudhuria mazishi ya Hayati Nelson Mandela kwa sababu ni ghali mno kusafiri hadi nchini Afrika Kusini, kwa mujibu wa taarifa za vyombo vya habari.

Awali, Bw Netanyahu alikuwa amefahamisha serikali ya Afrika Kusini kuwa angehudhuria mazishi hayo lakini akafutilia mbali safari hiyo katika dakika ya mwisho.

Kulingana na redio ya taifa la Israeli, waziri  huyo itatumia kiasi cha 7.0 milioni shekels ambazo ni sawa na Sh170 milioni kusafiri nchini Afrika Kusini pamoja na walinzi  wake:  “Uamuzi huo umeafikiwa kutokana na gharama kubwa ya usafiri kwani safari hiyo ilipangwa katika kipindi cha muda mfupi,” ikasema radio ya taifa, Haaretz.

Kiongozi huyo wa Israeli amekuwa akishutumia na raia wa nchi hiyo kuwa amekuwa akitumia zaidi ya dola $1 milioni kuendesha shughuli za kasri zake tatu. Vyombo vya habari vilidokeza kuwa kiongozi huyo hutumia fedha za walipa ushuru dola $23,000 kulipia maji  ya kujaza mabwawa ya maji.

Zaidi ya viongozi 70 kutoka kote duniani tayari wamethibitisha kuwa watasafiri kuelekea Afrika Kusini kwa ajili ya mazishi ya hayati  Nelson Mandela.

Kwa upande wake, mbali na kuwa shujaa ulimwenguni, Mandela pia anaashiria mwanzo mpya Afrika kwa kuleta pamoja kwa mara ya kwanza kongamano kubwa la viongozi ulimwenguni kando na Umoja wa Mataifa au Umoja wa Afrika.

Maishani mwake hadi kufariki kwake, Mandela ameweza kuendeleza ulimwengu. Maisha yake, kuanzia kufungwa kwake gerezani, kuchukua hatamu ya urais, kustaafu, hadi kufariki kwake, kumefanyika wakati ambapo kuna maendeleo makubwa ya kiteknolojia.

Mbali na televisheni na redio, magazeti na mitandao ya kijamii imeeneza habari kumhusu kwa kiwango kikubwa. Teknolojia imewezesha ulimwengu kuweza kuomboleza kwa pamoja, huku kila mmoja akiweza kuamua kuhusu watu wanaostahili kuombolezwa kwa taadhima kuu.

Hadhi kubwa inayoonekana katika maombolezo ya Mandela, ikiwemo idadi kubwa ya viongozi wa kitaifa wanaotarajiwa kuhudhuria, huenda isifikiwe na viongozi wengine katika karne hii.

Mandela, ambaye amecha watoto sita, wajukuu 17 na vitukuu 14, atazikwa nyumbani kwao Qunu, Cape Mashariki, Jumapili, Desemba 15.

0 maoni:

Post a Comment

waliotembelea blog