Saturday, October 19, 2013


Na Prudence Karugendo
WAKULIMA wengi wa kahawa wa mkoa wa Kagera, hususan walio chini ya chama kikuu cha ushirika cha KCU (1990) Ltd., wamezoea kuuza kahawa yao kupitia vyama vyao vya msingi kwa kutegemea bei wanayopangiwa na wanunuzi. Mnunuzi mkuu wa kahawa yao ni chama chao kikuu cha ushirika, KCU (1990) Ltd.. Chama hicho ndicho kinachowapangia bei wakul
ima kulingana na uongozi wake unavyojisikia.

Sababu hata kama bei ya kahawa inakuwa imepanda katika soko la dunia, kupanda uko kwa bei kutamnufaisha mkulima pale tu chama hicho kikuu cha ushirika kitakapokuwa hakina madai yanayokibana na hivyo kuhitaji kuyalipa, au matumizi mengine yanayotokana na uzembe unaosababishwa na uongozi bila kumhusisha mkulima kwa namna yoyote. Mkulima anajikuta tu akigeuka mwathirika wa uzembe ambao hakuushiriki.

Bei ya kahawa inaweza kupanda kidogo au ikashuka kabisa bila ya wakulima hao kuhoji lolote, hiyo ni kutokana na wakulima kuwachukulia viongozi wao wa ushirika kama miungu watu pasipokuelewa kuwa wao, wanaushirika, ndio waajiri wa viongozi hao.

Pamoja na vyama vya msingi kuwa na wawakilishi, walio na majukumu ya kuwasemea wanaushirika kuhusu mwenendo wa chama chao kikuu, bado hilo halikifanyi chama kikuu kuwathamini na kuwaheshimu wakulima, wanaushirika, kutokana na wawakilishi wao kuonekana wanajikomba sana kwa chama kikuu badala ya kukisimamia, kukielekeza pamoja na kukiwajibisha.

Sababu ya wawakilishi kufanya hivyo iko wazi, ni kwamba kila unapofika wakati wa wawakilishi kwenda kukisikiliza chama chao kikuu, chama hicho kinapanga mbinu za kila aina ikiwa ni pamoja na kuwakirimu wawakilishi hao.

Zinaandaliwa posho za ajabuajabu, hivyo wawakilishi wengi mawazo yao yanahamia kwenye posho na takrima za chama chao kikuu. Vitu hivyo vinawafanya wawakilishi wayaterekeze na kuyasahau majukumu yao. Kwa maana hiyo mwakilishi yeyote anayejaribu kutekeleza majuku yake ipasavyo anaonekana msaliti na baadaye kusakamwa na uongozi wa chama kikuu sambamba na wawakilishi wenzake.

Mfano wa karibuni ni wa Archard Felician Muhandiki, mwakilishi wa chama cha msingi cha Kamachumu, aliyefukuzwa kinyama kwenye mkutano mkuu wa hivi karibuni kutokana na kuuliza, pamoja na mambo mengine, kwa nini KCU (1990) Ltd. ilinunua hoteli ya Yasilla wakati hoteli yake ya zamani, Lake, ikioza.

Kwahiyo KCU (1990) Ltd, kinayachukulia matendo ya aina hiyo kama nafasi ya pekee kuweza kuyaburuza mambo jinsi kinavyotaka. Hakipati maswali muhimu wala uwajibishwaji kutoka kwa wawakilishi ambao kwa lugha nyingine ndio wakulima wanaounda ushirika.

Mara nyingi KCU (1990) Ltd. imeutumia uelewa mdogo wa wakulima kuhusu mambo ya ushirika na mengine yanayoambatana nayo, kwa manufaa yake. Mfano, ni wakulima wachache wanaoelewa masuala kama yale ya Soko la Haki “Fair Trade”, na kwa nini wanalipwa mara mbili wanapouza kahawa, yaani malipo ya awali na malipo ya mwisho.

Kwahiyo lengo la makala hii ni kuwaeleza wakulima, hasa wana KCU (1990) Ltd. kuhusu kitengo cha Moshi Export.

Baadhi ya wakulima wa kahawa wanakielewa kitengo hicho lakini walio wengi hawaelewi jinsi kinavyofanya kazi wala jinsi wanavyopaswa kunufaika nacho. Katika makala hii sintaeleza historia ya kitengo hicho, sababu hiyo iko katika makala nyingine nitakayoiandika, kwa hapa nitaeleza tu utendaji kazi wa KCU Moshi Export na jinsi kitengo hicho kinavyohujumiwa na makao makuu yake.

KCU Moshi Export ndicho kiungo kinachowaunganisha wakulima wa kahawa wa Kagera na wakulima wa kahawa wa kwingineko duniani. Kitengo hiki kina sifa nzuri sana nje ya nchi, na kwa sifa hiyo kahawa ya Kagera, na pengine ya Tanzania kwa ujumla, inakuwa imepata sifa vilevile. Hayo ni mafanikio yanayoibeba Tanzania katika kilimo cha kahawa wakati Tanzania nayo ikiwa imeibeba KCU (1990) Ltd. kwa mafanikio hayo.

KCU Moshi Export imeifanya KCU (1990) Ltd. iwe ya kwanza duniani katika kuuza kahawa aina ya robusta, ambayo wenyeji wa Bukoba wanaita “ emwani z’ekihaya”. Kahawa hiyo ndiyo inayotamba hata kwenye Soko la Haki “Fair Trade Market”.

Na kwa vile kitengo hicho cha Moshi ndicho kinachouza kwa kiwango kikubwa aina hiyo ya kahawa ndicho vilevile kinachopata kiwango kikubwa cha pesa kutoka kwenye Soko la Haki pamoja na pesa nyingine ya “social premium” kwa ajili ya kuendeleza maeneo inakolimwa kahawa hiyo.

Lakini hatahivo kuna dalili za wazi zinazojionyesha kwamba pesa itokayo kwenye Soko la Haki “Fair Trade” na kupelekwa kwenye chama kikuu ili kikapeleke kwenye vyama vya msingi, si vyama vyote vinaipata. Na kwa vile wakulima wengi wanao uelewa mdogo wa kitu hicho ni vigumu kuidai pesa hiyo wala kuiulizia.

Kitengo hicho cha KCU Moshi Export, mbali na nje ya nchi, pia kinayo sifa kubwa kitaifa. Hiyo inatokana na kitengo hicho kushinda vikombe mara tatu katika maonyesho mattatu tofauti ya hivi karibuni ya Nanenane kupitia Vyama vya Ushirika.

Jambo la kuzingatia hapa ni kwamba kitengo hicho cha Moshi sio tu kwamba kipo kwa ajili ya kuinadi kahawa itokayo KCU (1990) Ltd., bali pia ni kitegauchumi. Kinaingia kwenye mnada na kununua kahawa kwa kushindana na wanunuzi wengine hata wa kutoka nje ya nchi, kusudi kiweze kuiuza kahawa hiyo kwa bei ya juu zaidi na kuzalisha faida kwa ajili ya KCU (1990) Ltd.

Kwa utendaji kazi kilio nao kitengo hicho, ni wazi kabisa kwamba, kama KCU (1990) Ltd. kingekuwa kinaendeshwa kiuadilifu, hakipaswi kuwa na matatizo ya kifedha kama kiliyo nayo kwa sasa. Nisingetegemea kama KCU (1990) Ltd. kingekuwa kwenye msukosuko na benki ya CRDB kama ilivyo kwa sasa.

Ila maajabu yaliyopo ni kwamba kitengo hicho hakifanywi kujulikana sana kwa wakulima wa kahawa, wanaushirika wanaounda KCU (1990) Ltd.! Wanachama hao wanaachwa wakijue kitengo hicho kwa juujuu tu bila kuelewa kuwa ndicho kilicho mhimili mkuu uliokishikilia chama chao kikuu cha ushirika.

Kwahiyo utakuta kwamba viongozi wa ushirika huo ndio peke yao wanaotaka wakielewe kitengo hicho cha Moshi, ambako mara kwa mara wamekuwa wakichota pesa kwa ajili ya kuzibia mapengo yanayojitokeza, wakati mwingine, kwa njia za kizembe kabisa.

Kwahiyo badala ya KCU Moshi Export kuwanufaisha wakulima wa kahawa walio wanaushirika wa KCU (1990) Ltd. kimegeuzwa ni cha kuunufaisha uongozi wa ushirika huo uliogubikwa na uzembe, ambao kwa njia nyingine unajionesha kama ufisadi.

Hujuma ya KCU (1990) Ltd. dhidi ya kitengo chake cha Moshi (Moshi Export), imezidi kujionesha kwa wakati huu uliopo, baada ya chama hicho kikuu cha ushirika kuiachia benki ya CRDB, inayokidai chama hicho zaidi ya shilingi bilioni 5, izuie kahawa ambayo tayari imenunuliwa na kitengo hicho cha Moshi kwa ajili ya kusafirishwa nje ya nchi!

Sababu kwa maneno mengine ni kwamba kahawa hiyo sio tena mali ya chama hicho bali ni mali ya kitengo cha Moshi ambacho kiko kwenye makubaliano na wateja wa kimaifa wanaoisubiri kahawa hiyo toka kwenye kitengo hicho. La kuzingatia ni kwamba kitengo hicho cha Moshi tayari kimeilipia kahawa hiyo iliyoshikiliwa na CRDB kama dhamana ya mkopo unaodaiwa kwa chama kikuu.

Jambo linalojitokeza kama utapeli ni la kwamba kwa nini chama hicho kikubali kuigeuza dhamana mali ambayo tayari kimeiuza?

Pamoja na hayo yote, la kutilia mkazo ni kwamba wakulima wa kahawa, au niseme wanaushirika wote wa KCU (1990) Ltd. wanapaswa waelezwe na waelewe jinsi kitengo cha KCU Moshi Export kinavyofanya kazi, pia waelezwe kuhusu Soko la Haki (Fair Trade Market) na namna pesa inayotokana na soko hilo inavyofanya kazi. Haifai hata kidogo waendelee kuuziwa mbuzi kwenye gunia.

Kwa vyovyote ilivyo, KCU (1990) Ltd., ni ushirika unaojinyonga wenyewe hasa baada kuonekana unakihujumu kitengo chake ambacho ni kitega uchumi chake kikuu, KCU Moshi Export.

0 maoni:

Post a Comment

waliotembelea blog