SIMBA SC imefanya mkutano mkuu wa kawaida wa
wanachama Agosti 3 mwaka huu katika ukumbi wa Bwalo la Maofisa wa Polisi,
Osterbay, jijini Dar es salaam ambapo Agenda 13 zilijadiliwa.
Moja ya Agenda muhimu katika mkutano huo ilikuwa
ile ya wanachama 72 waliosimamishwa uanachama akiwemo Michael Richard Wambura na
mabadiliko ya katiba.
Kabla ya kufanya uchaguzi mkuu wa Simba juni 29
mwaka huu uliomuingiza madarakani Rais Evans Elieza Aveva, klabu hiyo ilifanya
mabadiliko ya katiba yake.
Katika mabadiliko hayo kiliwekwa kipengele cha kumruhusu
mtu aliyewahi kufungwa huko nyuma kupata nafasi ya kugombea. Watu wengi
yawezekana hawafahamu siri iliyofichika katika mabadiliko ya kipengele hiki.
Baadhi ya wanachama walioona umuhimu wa Zacharia Hans
Poppe ambaye aliwahi kufungwa huko nyuma kwa makosa ya uhaini, waliweka kipengele
kwamba mtu aliyefungwa agombee kwenye katiba ya Simba.
katika mkutano mkuu wa mabadiliko ya katiba,
wanachama wakapitisha kipengele hicho, lakini ilipofika TFF kule, kile
kipengele kikaminywa na hakikupitishwa.
Kwa utaratibu, Katiba inatakiwa TFF waipitishe,
lakini ilipoenda kule wakabana kipengele hicho na hii ni kwasababu TFF kuna
viongozi wa Simba ambao hawakutaka Hans Poppe apate nafasi ya kugombea.
Baadhi ya watu waliokuwa na nia ya kugombea nafasi
za uongozi wa juu, hawakupendezewa na kipengele hicho kuwekwa ambacho kilikuwa
kinamruhusu mwenyekiti wa kamati ya usajili wa klabu hiyo, Keptein wa zamani wa
Jeshi la wananchi Tanzania, (JWTZ), Zacharia Hans Poppe kugombea.
Mkutano
mkuu wa mabadiliko ya katiba ya Simba ulipitisha kipengele cha kuruhusu
mtu aliyefungwa huko nyuma kugombea, lakini TFF waligoma kukupitsiaha
Hans Poppe ni mtu anayestahili kuwa kiongozi wa
Simba kwasababu ana sifa zote. Ni mwanachama halisi, anajitolea kwa moyo wote
kuisaidia klabu, yaani ana mapenzi ya dhati. Yupo tayari kuisaidia timu bila
kunufaika na chochote.
Yeye ni tofauti na wale ambao wanajihusisha na
timu ili waweze kufanya biashara zao. Hans Poppe hahitaji kufanya biashara na
Simba zaidi ya kujitolea na kuisaidia timu kutokana na mapenzi ya dhati
aliyokuwa nayo.
Kilichonikera mimi, ni kitendo cha wanachama hao
hao wa Simba na baadhi ya watu ambao ni mahiri kabisa kujifanya wanaipenda
Simba, lakini kumbe hawaitakii Simba mema na wapo kwa ajili ya kupata umaarufu
au manufaa mengine kwa kutumia fursa ya kuwepo klabuni hapo.
Ule mkutano mkuu wa katiba ulipitisha kipengele
cha kumruhusu Hans Poppe aweze kugombea, lakini kuna watu TFF wakaamua kuweka
zengwe na kugoma kupitisha.
Zacharia Hans Poppe ana sifa zote za kuwa kiongozi wa Simba sc
Nimesema awali kuwa kule TFF kuna viongozi wa
Simba ambao walikuwa na nia ya kugombea Urais, kwahiyo wakabana kupitisha
kipengele cha kumruhusu Hans Poppe kwasababu waliona atakuwa ni kikwazo kwao.
Wakaenda mbali zaidi na kuweka kipengele katika
katiba ya Simba kuwa hata wale wajumbe watano watakaoteuliwa na Rais, lazima
wawe na sifa kama zile za wajumbe waliochaguliwa na wanachama.
Uchaguzi
ukafanyika na Hans Poppe akatolewa. Lakini Hans Poppe huyo huyo pamoja na
kufanyiwa hizo hila, alionesha kuwa yeye ni mwanachama halisi na mpenzi wa
Simba na alitoa milioni 20 kwa ajili ya kuendesha mkutano mkuu wa uchaguzi wa Simba.
Ule mkutano mkuu wa Simba usingefanyika kama Hans
Poppe asingetoa hela hizo. Aliyafanya
haya wakati tayari alishawekewe mizengwe na angekuwa mtu mwingine, angesusa na
kuondoka zake, lakini alisaidia uchaguzi ufanyike.
Unafiki wa viongozi wa mpira wa Tanzania, uongozi
uliokuwepo madarakani chini ya mwenyekiti wake, Ismail Aden Rage, kwenye mkutano ule wa uchaguzi ulisema kwamba
umeacha hela kwenye akaunti na hauna madeni, lakini kiuhalisia uongozi huo
ulikuwa unadaiwa na Hans Poppe zaidi ya milioni 250 na mpaka sasa hajaidai
klabu.
Hizi ni pesa ambazo alikuwa akizitoa kwa ajili ya
kusaidia masuala ya usajili kwasababu yeye alikuwa mwenyekiti wa kamati hiyo na
zingine ilikuwa ni kwa ajili ya kuendesha shughuli za kila siku za klabu.
Kabla ya uchaguzi, vilitengenezwa vipengele vya
kumruhusu Hans Poppe kugombea na katiba ilipofika TFF wakaminya, lakini baada
ya malengo yao kufanikiwa kwa kumuwekea vigingi, sasa wanaona aibu na kuitisha
mkutano mkuu wa wanachama ili kufanya mabadiliko ya katiba, ikiwa ni siku
chache tu baada ya kuingia madarakani.
Zacharia Hans Poppe (wa kwanza kulia) alikuwepo katika uongozi uliomaliza muda wake chini ya mwenyekiti Ismail Aden Rage.
Huo mkutano ulikuwa ni kubadili kipengele kimoja
tu ili kuweza kumsafisha Hans Poppe aweze kuwa na sifa ya kuteuliwa kwenye
kamati ya utendaji.
Kwahiyo kile kipengele kilichowekwa kwa ajili ya
kumruhusu na kikaminywa, ndio kile kile
kikasababisha uitishwe mkutano mkuu ili kirekebishwe na kumpa Rais mamlaka ya
kuteua wajumbe wa kamati ya utendaji pasipo kuzingatia sifa za hapo awali.
Kipengele kinabadilishwa na wale wanaohitaji
‘mahela’ ya Hans Poppe ili awasajilie wachezaji, lakini anarudije wakati amewekewa
kipengele cha kumzuia?
Hapo ndipo mkutano wa wanachama uliitishwa ili
kutegua ule mtego tena. Wanahangaika kutegua mtego ili Hans Poppe awe huru na
kuweza kuingia kamati ya utendaji.
Simba hao hao wakiwa kule TFF walimuweka kwenye mtego
wa Panya, na sasa wanahangaika kuutegua ili aweze kutoka. Simba walidhani Hans
Poppe ni panya, lakini wamekuja kugundua sio panya.
Zacharia Hans Poppe akiwa ofisini kwake
Mimi binafsi namkubali Hans Poppe, bila mizengwe,
chuki wala fitina, na naamini ana sifa za kuwa kiongozi wa Simba
ni aina ya watu wanaostahili kuiongoza Simba,
lakini kuna watu wengine ambao hawahitaji kuona maslahi ya Simba na wanamuona
yeye kama kikwazo.
Wanahangaika kumrejesha, kwahiyo wanang`ata huku
na kupuliza. Huu ni unafiki usiotakiwa kuwepo na wakubali kuwa Hans Poppe
anastahili kuwepo Simba na wasiweke mizengwe, wabadili kabisa katiba na
kumfanya siku za usoni awe Rais wa timu kwasababu ana uwezo.
Isije ikafika muda wa uchaguzi, wakaitisha tena
mkutano wa kufanya mabadiliko ya katiba ili Hans Poppe asigombee.
Halafu kuna kipengele kingine cha nafasi ya wazee
wa klabu. Katiba ya Simba inasema, lazima mmoja wa wazee wa klabu aingie katika
kamati ya utendaji, lakini wazee wote wa Simba waliopo, yawezekana hawana sifa kama
zile za wagombea.
Kwahiyo wanatoa kipengele hicho ili kuruhusu mmoja
wa wazee kuingia kwenye kamati ya utendaji.
Ina maana hao wazee wa Simba ambao hawana sifa
wamezaliwa wao tu na hakuna nafasi ya kutafuta wazee wengine ambao wana sifa
kama za wagombea?
Ina maana wazee wote wanaoipenda Simba hawajamaliza
kidato cha nne? Yaani wazee wote duniani ambao wamejitolea kwa ajili ya Simba
hawana vyeti vya kidato cha nne?
Au kwanini wasifanye mabadiliko ya katiba kama
wanagundua kuwa wazee hawana sifa zile za wagombea ili iwe kwamba, sio lazima
kwenye kamati ya utendaji awepo mzee.
Kiukweli hakuna mashiko kwa kipengele hiki cha
wazee. Hapa ni kujaribu kuficha ukweli, sababu ya mabadiliko ya katiba itabaki
kuwe ile ile ya kutafuta namna ya kumuingiza kwenye mfumo Hans Poppe.
Binafsi bila kumung`unya maneno, Zacharia Hans
Poppe ana kila sifa ya kuwa kiongozi ndani ya klabu ya Simba.
Umefika
muda sasa wa Unafiki, mizengwe, uzandiki kupigwa vita na kukemewa
michezoni kama kweli tuna nia ya dhati ya kuendelea kufanya vizuri katika
mashindano mbalimbali.
Moja kati ya sababu kubwa inayokwamisha sola la
Tanzania kuendelea ni unafiki na uzandiki uliojaa kwa viongozi wa nchi hii.
0 maoni:
Post a Comment