Saturday, February 15, 2014


Simba

Mbeya City

JIJI la Mbeya leo litasimama kwa muda wakati wenyeji Mbeya City watakapoikaribisha Simba kwenye uwanja wa Sokoine likiwa ni moja ya michezo ya Ligi Kuu Tanzania Bara inayochezwa leo nchini.
Mechi hiyo inavuta hisia kubwa kuliko hata mechi za kimataifa ambazo timu za Yanga na Azam zilizopo ugenini zitakuwa zikiiwakilisha Tanzania katika kutafuta nafasi ya kufuzu raundi ya kwanza.
Mvuto wa mechi hiyo ya Mbeya unatokana na ukweli kuwa Simba katika mechi zake mbili zilizopita ilionekana kupepesuka, huku Mbeya City inayotajwa kuwa tishio zaidi ikiwa uwanja wa nyumbani ikiwa na kumbukumbu ya kupata sare dhidi ya Mnyama katika mechi yao ya duru la kwanza jijini Dar es Salaam.
Mashabiki wa Mbeya wanaamini Simba leo haitatoka kama walivyoifanyia Mtibwa Sugar au ilipoibana Yanga ilipoenda kucheza nao kwenye uwanja huo mwaka jana.
Hata hivyo mashabiki wa Simba wenyewe wanaamini wameenda Mbeya ili kukata mzizi wa fitina wa kutofungika kwa timu hiyo kwenye uwanja wao wa nyumbani na kutaka kuendeleza ilichokifanya Yanga kwa 'kuitengua udhu' walipoumana nao wiki mbili zilizopita jijini Dar na kuzima rekodi ya kutofungika kabisa licha ya kucheza Ligi Kuu kwa maraya kwanza msimu huu.
Makocha wa timu zote mbili wamenukuliwa wakitambiana kwamba leo ni leo, lakini kwa kuwa mpira ni dakika 90 mashabiki watakuwa na hamu ya kuona mechi hiyo itaishaje.
Simba chini ya makocha Zdrakov Lugarusic na msaidizi wake, Seleman Matola wameapa kupata ushindi ili kurejea kwenye nafasi ya tatu waliyoikalia kwa muda kabla ya Mbeya City kuirejea na kuirudisha Simba nafasi ya nne iliyokuwa inaikamata tangu duru la kwanza lilipoisha.
Mbeya City nayo chini ya kocha Juma Mwambusi wameapa kutaka kuizima Simba ili kunyakua pointi tatu na kuzidi kusonga nafasi za juu ili kutimiza ndoto za kutaka kunyakua ubingwa wa Ligi Kuu katika msimu wao wa kwanza kama walivyowahi kufanya 'kaka' zao Tukuyu Stars mwaka 1987.
Timu zote zinawategemea nyota wao kadhaa, Simba ikimtambia kinara wa mabao Amissi Tambwe, Ramadhani Singano 'Mess' na Haruna Chanongo, wakati Mbeya City inayoundwa na vijana zaidi ikiwategemea 'wauaji' wao Mwagani Yeya, Paul Nonga, Jeremiah Michael na mkongwe Stephen Mazamba.
Mbali na mechi hiyo iliyo gumzo kwa mashabiki wa soka nchini kote kwa sasa, leo pia kutakuwa na mechi nyingine tano, ambapo Ruvu Shooting itaikaribisha Coastal Union kwenye uwanja wa Mabatini-Mlandizi Pwani, huku Mgambo JKT itakuwa ugenini dhidi ya Rhino Rangers.
Mechi nyingine itazikutanisha timu za Oljoro JKT itakayokuwa uwanja wake wa nyumbani wa Sheikh Amri Abeid kuvaana na maafande wenzao wa JKT Ruvu, huku Ashanti Utd wataialika Kagera Sugar kwenye dimba la Chamazi  jijini Dar es Salaam na Mtibwa Sugar itaikaribisha Prisons-Mbeya uwanja wa Manungu.


0 maoni:

Post a Comment

waliotembelea blog