Sunday, July 7, 2013

ULEVI KWA WATU WENYE WANAOUGUA MARADHI YA UGONJWA WA UKIMWI NI HATARI. 

ULEVI miongoni mwa watu wenye Virusi Vya Ukimwi (VVU) umeelezwa kuwa ni hatari kwani pombe inaharibu mfumo wa kinga mwilini na kupunguza chembe hai za kinga -CD4 na kusababisha virusi kuzalishwa kwa wingi. 


Chembe za CD4 ni jeshi la kingamaradhi linalohusika na kukabiliana na magonjwa wakati mwili unapogundua kuna virusi au vimelea vya magonjwa.

Kwa mujibu wa kipeperushi cha madhara ya Pombe kwa Wenye VVU kilichoandaliwa na Mpango wa Taifa wa Kudh
ibiti Ukimwi (NACP), aidha kuchanganya dawa za ARV na pombe kunasababisha usugu na kuzalisha virusi hatari zaidi.

Pia, NACP ilisema pombe inasababisha madhara kwenye ini na kwamba baadhi ya dawa za Ukimwi ili zifanye kazi kikamilifu ni lazima zipitie kwenye ini na kwa mlevi linaweza kuwa na matatizo.

NIPASHE Jumapili ilifuatilia athari za ulevi kwa wenye VVU baada ya kupokea taarifa za baadhi ya watoa huduma wanaofuatilia mwenendo wa wagonjwa wa Dar es Salaam na mikoa ya jirani zikieleza kuwa wapo watu hunywa pombe licha ya kutumia dawa.

Walieleza kuwa baadhi ya watumiaji dawa wanabadili ratiba kwa kunywa vidonge asubuhi, wakati mwingine wanachanganya na kumeza dawa za mchana na usiku ili waende vilabuni kunywa pombe jioni.

Watoa huduma walisema wagonjwa huacha kunywa dawa kwa mujibu wa maelekezo jambo walilosema linakwamisha mikakati ya tiba.

”Utawakuta wanakimbilia kunywa komoni, kimpumu hata gongo” alisema mtoa huduma wa kituo cha afya kilichoko mkoani Pwani.

Wahudumu wengine waliozungumzia ukiukwaji wa masharti ya kumeza ARV walishauri kutoa dawa hizo chini ya usimamizi wa mtaalamu wa afya kama inavyofanyika kwa watumiaji wa dawa za kifua kikuu (TB) na kuandaa muongozo wa Wizara ya Afya unaoelekeza matumizi ya dawa na kukataza ulevi.

Walisema baadhi ya wagonjwa hupendelea pombe kwa madai kuwa hawaogopi kifo kwani wao ni “marehemu japo wanaishi” na wakidai ARV zina madhara mengine mwilini.

 

0 maoni:

Post a Comment

waliotembelea blog