Safari ya Rais KIkwete Sunderland huenda ikawa mwisho wa kiu ya mpira Tanzania
Jumapili iliyopita nilibahatika kuwa ndani ya msafara mahususi uliozunguka na mheshimiwa Rais Jakaya Kikwete.
Ingawa msafara huo ulihusu michezo na mpira,
uliwakutanisha pia baadhi ya Watanzania wakazi wa Jiji la Sunderland na
wale wasomao Chuo Kikuu cha New Castle, Kaskazini Mashariki ya Uingereza
Rais Kikwete alipotua jijini Sunderland jua
lilikuwa liking’ara, saa za adhuhuri...Mwezi wa sita huwa kiangazi ndiyo
kinaanza anza Ulaya hivyo siyo lazima kuvaa makoti mazito. Mkuu wa nchi
alikuwa nadhifu na wasaizidi wake kama kawaida, akiwemo Waziri wa
Habari, Utamaduni, Vijana na Michezo, Dk Fenella Mukangara, Balozi wetu
hapa Peter Kallaghe na maofisa wengine husika walichangamkia shughuli
hii muhimu na ya kihistoria, kama tutakavyoona.
Upande wa wenyeji je?
Mmiliki klabu ya Sunderland ni tajiri wa
Kimarekani, Ellis Short kipato chake kinakisiwa kuwa Dola za Marekani
3.5 bbilioni, ndiye alimwalika Rais Jakaya Kikwete na Paul Hinks,
Mwendeshaji Mkuu wa Kampuni ya Ujenzi Umeme ya Symbion Power, yenye
makao Marekani. Pande hizi mbili ndizo zitashirikiana, moja kujenga
Symbion chuo cha kufundishia watoto mpira, mwingine kutoa mafunzo hayo
Sunderland AFC.
Kwa vipi klabu iliyochukua nafasi ya 17 mwaka huu
ndani ya Ligi ya Uingereza kati ya timu 20, ichaguliwe kutufariji,
aliulizwa Rais Kikwete baadaye na wanahabari? Kwa nini wasiwe Arsenal,
Chelsea, Liverpool au watemi wa Manchester United?
Rais Kikwete akajibu ilitokana na Ellis Short
mwenyewe kuitembelea Tanzania kwa shughuli zake nyingine; Hapo msosi
ukatayarishwa. Sunderland inasifika kwa kituo chake bora kufunzia watoto
kiitwacho “Academy of Light.” Ukichunguza sana maendeleo ya wachezaji
wote wakubwa duniani, huanzia vilabu vidogo ndiyo wakanunuliwa na
hatimaye kutamba na timu zenye fedha na uwezo zaidi. Mfano mzuri ni
wanasoka maarufu wa ligi ya Uingereza Theo Walcott (Arsenal) Oxlade
Chamberlain( Arsenal ) na Gareth Bale wa Tottenham walioanzia mpira
utotoni Southampton Football Academy.
Sidhani ni wengi tunaoijua au kuisikia,
Southampton, barani Afrika. Lakini huu ni ushahidi wa namna klabu ndogo
zisizojulikana zinavyoivisha na kumeng’enya wachezaji chipukizi. Gareth
Bale sasa hivi anapiganiwa na kila klabu na inasemekana Real Madrid
wanamtamani kwa mate na udenda. Hata kwetu Bongo wachezaji wengi huanzia
klabu ndogo za mikoani kabla ya kununuliwa Simba na Yanga.
Hivyo Sunderland inaweza isiwe kubwa, lakini uwezo
wake wa kiufundi utaikidhi sana Tanzania. Msafara wa Rais ulionyeshwa
eneo hili kubwa lililokamilika miaka kumi iliyopita. Humo mna sehemu za
kuogelea, viwanja vyenye majani safi ndani na nje, Gym za mazoezi,
madarasa na vyombo mbalimbali vya mafunzo. Mbali na chuo, Rais Kikwete
alitembezwa uwanja wa “Stadium of Light” ambao hujaza watazamaji 49,000.
Huu ni uwanja wa tano kwa ukubwa Uingereza nzima. Hapa huwepo vilevile
maonyesho siyo madogo ya muziki, kama lile la mwimbaji nguli Rihanna
toka Barbados aliyetumbuiza juzi Alhamisi.
Kuna hilo la kiufundi, halafu historia.
Si wengi wanaofahamu historia za vilabu vyetu.
Rais alipowaeleza wanahabari wa Kizungu kuwa
zamani Simba ilipoanzishwa mwaka 1936 iliitwa Dar Sunderland, alikuwa
akikumbusha tulikotoka.
0 maoni:
Post a Comment