Thursday, July 9, 2015


KLABU ya BidVest Wits ya Afrika Kusini ambayo hivi karibuni iliwaalika Simon Msuva wa Yanga SC na Jonas Mkude wa Simba SC kwa majaribio, imemsajili winga wa kimataifa wa Msumbiji, Elias Pelembe (pichani) kutoka Mamelodi Sundowns.
Pelembe amemaliza mkataba wake na 'Wabrazil' mwezi uliopita na baada ya kufanya mazungumzo na klabu kadhaa, akaamua kuungana na Gavin Hunt klabu ya Wits.
Klabu hiyo imetweet leo juu ya kumsajili mchezaji huyo na wazi hilo ni pigo kwa Kaizer Chiefs na Orlando Pirates ambazo nazo zilikuwa zinamtaka mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 31.
Pelembe alicheza kwa mara ya kwanza chini ya Hunt wakati alipojiunga na SuperSport United msimu wa 2007/2008 akitokea Desportivo Maputo ya Msumbiji.
Alishinda mataji mfululizo na Matsatsantsa kabla ya kuhamia Sundowns mwaka 2009, akiripotiwa kuwa miongoni mwa wachezaji wanaolipwa zaidi Ligi Kuu ya Afrika Kusini.
Baada ya misimu sita ya wawili hao kuwa tofauti, hatimaye Hunt anakutana tena na Pelembe Wits.
Pelembe, anayecheza kulia, anakuwa winga wa pili kununuliwa na klabu hiyo msimu huu baada ya Daine Klate aliyejiunga na timu hiyo Juni. Klabu hiyo pia imemsajili beki mkongwe Nazeer Allie kutoka Ajax Cape Town.

0 maoni:

Post a Comment

waliotembelea blog