Saturday, November 15, 2014


David Moyes, Meneja alietimuliwa Manchester United Mwezi Aprili Mwaka huu, ametua rasmi huko San Sebastián Nchini Spain kujiunga na Real Sociedad kama Meneja wao mpya.

Mara baada ya kutua kwenye Klabu hiyo ya La Liga ambayo Jina lake la ubatizo ni La Real, Moyes alikiri kuwa kabla hajakubali rasmi kujiunga na Real Sociedad alimtaka ushauri Sir Alex Ferguson ambae alimbariki kuchukua nafasi hiyo.

Feguson, ambae alistaafu kuwa Meneja wa Man United Mei Mwaka Jana baada ya himaya ya Miaka 26 na kubakia hapo kama Mkurugenzi, ndie aliependekeza mrithi wake awe David Moyes.

Akikiri kuwa hadi hii leo ni marafiki, Moyes alieleza: “Niliongea na Sir Alex na akaniambia hii ni nafasi nzuri.”

Moyes pia alikumbushia himaya yake ya Miezi 10 Old Trafford na kusisitiza hakupewa muda wa kutosha.

Moyes, ambae kabla ya kujiunga Man United alikuwa Meneja wa Everton, amesisitiza ni ngumu kwa Mtu yeyote kumrithi Sir Alex Ferguson.
Lakini pia Moyes amesema uzoefu wake na Man United utaisaidia sana Real Sociedad.
Huko Real Sociedad Moyes anambadili Jagoba Arrasate aliefukuzwa Wiki 2 zilizopita baada ya matokeo mabovu ambayo yameifanya Klabu hiyo iwe Nafasi ya 15 kwenye La Liga.
Moyes amesaini Mkataba hadi Juni 2016 na Mechi yake ya kwanza kama Meneja ni hapo Novemba 22 watakapocheza ugenini Mechi ya La Liga na Deportivo La Coruna.

Kwa Real Sociedad Moyes anakuwa Meneja wa nne kutoka Uingereza katika historia yao na wengine waliowahi kuongoza Klabu hiyo ni Harry Lowe aliekaa huko Miaka 5 kuanzia 1930, John Toshack aliekaa kwa vipindi vitatu tofauti na Chris Coleman alieteuliwa Julai 2007 na kudumu Miezi 7 tu.

Msimu huu kwenye Ligi, licha ya kusuasua, Real Sociedad tayari wamewafunga Vinara wa La Liga, Real Madrid, na Jumapili iliyopita kuwatwanga Mabingwa Watetezi Atletico Madrid Bao 2-1.

0 maoni:

Post a Comment

waliotembelea blog