Na Baraka Mpenja, Dar es salaam
KOCHA mkuu wa Mbeya City fc na kocha bora wa ligi
kuu Tanzania bara msimu uliopita, Juma Mwambusi, amewakaribisha makocha Patrick
Phiri wa Simba na Marcio Maximo wa Yanga.
Akizungumza mchana huu na MPENJA BLOG, Mwambusi amesema
kocha Phiri ana historia ya kufundisha soka la Tanzania kwa ngazi ya klabu
wakati Maximo amefundisha timu ya Taifa, lakini wote wataleta changamoto nzuri
kwake.
Mwambusi aliongeza kuwa ujio wa makocha wapya
unaleta vionjo vipya katika ligi, lakini yeye kama mwalimu anajipanga
kukabiliana kwa nguvu zote ili kuendeleza mafanikio ya msimu uliopita.
“Mimi naona tungoje dakika 90 zitakuwa zinatoa
majibu. Sina la kusema zaidi ya kusema ni changamoto. Mwalimu mpya anapopatikana
katika ligi anakuja na kionjo kipya, kama mwalimu lazima ukabiliane nacho.
Kwahiyo sisi tunawakaribisha ligi kuu Phiri na Maximo.” Alisema Mwambusi.
Aidha, Mwambusi alifafanua kuwa maandalizi ya ligi
kuu yanakwenda vizuri na wapo hatua za
mwisho kabisa kuhakikisha wanapata kikosi cha kwanza.
Alisema mwishoni mwa wiki hii wanatarajia kupata
mechi ya mwisho ya kirafiki itakayofunga mahesabu ya kuanza msimu mpya
unaotarajia kuanza septemba 20 mwaka huu.
“Vijana wanaendelea vizuri na tuko katika
kumalizia-malizia maandalizi na tunaangalia utaratibu wa kupata timu ya kucheza
mechi ya kirafiki ili kupata kikosi cha kwanza”
“Wachezaji wote wako katika hali nzuri, kikubwa
tunadhani mwishoni mwa wiki hii tutakuwa na mechi ya kirafiki ambayo
itakamilisha maandalizi yetu na tujue tunatokaje katika mechi za ligi kuu.”
“Bado viongozi wanafanya jitihada kupata timu kutoka Malawi na ikishindikana
tutacheza na timu ya hapa ndani ambayo itatupa upinzani mzuri”
Kocha huyo
maarufu kwa sasa alisema soka sio mchezo wa kutabiri, lakini anashukuru kwa
vile mwaka jana walitoa changamoto kubwa na timu nyingi zinataka kuwaiga wao.
“Mpira wa miguu sio wa kutabiri, lakini mimi
nashukuru kwa kuwa mwaka jana Mbeya City fc tumeleta changamoto na watu
wanajiandaa vizuri sana na kila mtu anataka kuona timu yake itafanyeje ili
iweze kuwa kama Mbeya City. Mimi nafikiri ligi itakuwa na changamoto sana mwaka
huu.
Msimu uliopita, Mbeya City ilishika nafasi ya tatu
kwa pointi 49 nyuma ya Yanga walioshika nafasi ya pili na Azam fc nafasi ya
kwanza (mabingwa).
Mbeya city wanatarajia kuanza kampeni zao za kusaka ubingwa msimu wa 2014/2015 septemba 20 mwaka huu katika uwanja wa nyumbani wa Sokoine jijini Mbeya dhidi ya maafande wa JKT Ruvu.
0 maoni:
Post a Comment