Saturday, August 23, 2014



Kocha mkuu wa Yanga sc (katikati), Mbrazil Marcio Maximo amewasili kisiwani Unguja kuendelea kuiwinda ligi kuu Tanzania bara

Na Baraka Mpenja
BAADA ya kukamilisha programu ya mazoezi ya siku tano kisiwani Pemba, kikosi cha Yanga kimewasili kisiwani Unguja (Zanzibar) tayari kwa kumalizia siku nyingine tano zilizosalia.
Yanga imeweka kambi ya siku 10 Zanzibar na tayari imekata tano ikiwa pemba ambapo ilicheza mechi moja ya kirafiki dhidi ya Chipukizi FC katika uwanja wa Gombani na kushinda bao 1-0.
Bao hilo pekee lilifungwa na mshambuliaji Mbrazil Geilson Santos Santos Santana ‘Jaja’ katika dakika ya 6 ya mchezo.
Katika mechi hiyo iliyokuwa ya kwanza kwa kocha mkuu, Mbrazil Marcio Maximo, Yanga ilitumia vikosi viwili tofauti kwa kila kipindi.
Ikiwa kisiwani Unguja, kesho Yanga inatarajia kucheza mechi ya kirafiki dhidi ya Shangani FC majira ya saa 10:00 jioni uwanja wa Aman mjini Zanzibar.
Hii itakuwa mechi nyingine muhimu kwa Maximo kuona kama wachezaji wake wamefuta makosa ya mechi ya Gombani au hapana, ili ajue nini cha kufanya zaidi kabla ya kuanza kwa msimu mpya wa ligi septemba 20 mwaka huu.
Wakati huo huo Mahasimu wao, Simba chini ya kocha Patrick Phiri wapo mjini Unguja wakiendelea na mazoezi yao.
Leo Simba walifanya mazoezi kidogo ili kuiandaa miili ya wachezaji kwa ajili ya mechi ya kwanza ya kirafiki kesho uwanja wa Aman dhidi ya Kilimani FC.
Kocha mkuu wa Simba akiongea na wachezaji wake
Mechi hii itapigwa majira ya 2:00 usiku saa chache tu  kupita baada ya kuishuhudia  Yanga ikicheze katika uwanja huo huo.
Mechi hizo zitatoa burudani kwa mashabiki wa Yanga na Simba visiwani Zanzibar kwasababu watazishuhudia timu zao zikicheza uwanja mmoja kwa kupishana saa chache.
Kocha wa Simba kwa muda mrefu sasa amekuwa akiwafundisha vijana wake jinsi ya kumiliki mpira, kukaba kwa mipango na kushambulia kwa kasi.
Lengo la Phiri ni kuifanya Simba kuwa bora katika maeneo hayo matatu kabla ya kuanza ligi kuu.
Simba wataanza kucheza mechi nyingi nyumbani ambapo mechi ya ufunguzi Septemba 21 uwanja wa Taifa watachuana na Wagosi wa Kaya, Coastal Union ambao nao wako Pemba kujifua.

Yanga wao wataanza kampeni ya kusaka ubingwa septemba 20 katika dimba la Jamhuri mkoani Morogoro dhidi ya wakata miwa wa Mtibwa Sugar.

0 maoni:

Post a Comment

waliotembelea blog