Simba itarudia rekodi ya 1993 barani Afrika?: Rais wa Simba sc, Evans Elieza Aveva anaaminiwa kurudisha heshima ya klabu hiyo.
Na Baraka Mpenja, Dar es salaam
0712461976
MZAMBIA Patrick Phiri huwezi kuthubutu kumdharau
hata kwa dakika moja, hakika ni miongoni mwa makocha wa kigeni waliopata
mafanikio makubwa wakifundisha klabu za ligi kuu soka Tanzania.
Phiri ni kocha mwenye heshima kubwa ndani ya klabu
ya Simba na sasa amekabidhiwa majukumu ya kuinoa timu kuelekea msimu ujao wa
ligi kuu unaotarajia kuanza septemba 20 kufuatia aliyekuwa kocha wa klabu hiyo,
Mcroatia, Zdravko Logarusic kuachishwa kazi.
Kilichomuondoa Loga sio uwezo mdogo wa kitaaluma.
Huyu ni kocha wa kiwango cha juu, lakini sababu ilikuwa ndogo tu, tabia,
matendo na mitazamo yake ambayo haikuonekana kuijenga Simba sc.
Siwezi kumkosoa Loga moja kwa moja kwa ukali wake
kwa wachezaji na misimamo yake kwa viongozi au tabia ya nje ya uwanja kwasababu
nafahamu kuwa kocha yeyote lazima awe na falsafa yake ya kufanya mambo yake.
Falsafa ya mwalimu huwa haibadiliki. Kama anaamini
ukali kwa wachezaji ni suala zuri kwake, basi atasimama hapo hapo. Kama
anaamini kuwatumia vijana zaidi kuliko ‘Mafaza’ basi inabidi aachwe afanye kazi
yake.
Kuipinga falsafa ya mwalimu ni kuingilia taaluma
yake. Kinachotakiwa ni kuangalia kama falsafa yake inaisaidia timu, kama ni
hapana, lazima aondolewe mara moja, kama ni ndiyo apewe muda na kuaminiwa.
Najua Loga yupo sahihi kwa mitazamo yake kwasababu
kuna sehemu inaweza kufaa, lakini kwa utamaduni wa Simba na soka la Tanzania na
maeneo mengine Duniani yawezekana haifai.
Nimekuwa nikimkubali Loga kwa wakati wote
linapofika suala la nidhamu kwa wachezaji. Anawasimamia na kuwafanya wajielewe
na kujituma, lakini tatizo langu lipo kwenye namna anavyowasimamia.
Loga hakuwa rafiki kwa wachezaji. Alikuwa mkali
mno na hili lipo wazi. Tatizo la msingi lilianzia hapo, sidhani kama Simba
walikuwa na tatizo kwa yeye kukazania nidhamu, lakini tatizo lilikuja pale alipoanza
kuwatukana watu wazima kama ‘Baba wawili’ Amri Kiemba na Shaaban Kisiga na
wengineo.
Utanyanyua
tena msimu ujao?: Makamu wa Rais wa Simba, Geofrey Nyange 'Kaburu'
Perez akionesha moja ya kombe la Ubingwa wa klabu hiyo
Unaweza kuwa sahihi katika jambo fulani, lakini
namna ya kulitenda ikawa tatizo. Hii ni sawa na haki ya msingi ya kila mtu kutoa maoni na kukosoa kitu au jambo
fulani.
Ni vizuri kukosoa au kukosolewa, hakuna tatizo juu
ya hili, lakini namna ya kukosoa ndio inafanya mtu asikuelewe na kuona una
chuki binafsi, umetumwa au kwa lugha nyepesi una lako jambo.
Ukosoaji ninaopenda mimi ni kutoa hoja mbadala.
Sipendelei kauli kama hapo umekosa sana, huna lolote, hii ndio Bongo, hawa ndio
viongozi wa soka letu, huwa napenda kusikia mtu anaanika kosa na kutoa
suluhisho.
Kama viongozi wa Simba na Yanga wanakosea,
waambie, kisha wape njia mbadala ya kufanikiwa. Wakisikiliza, wasiposikiliza
sawa, maoni sio sheria na ndio maana yakaitwa maoni na sio agizo.
Kwa bahati mbaya sana, wengi wetu si wazuri wa
kutoa hoja mbadala. Unaweza kumsikia mtu anasema Loga hafai kabisa kuiongoza
Simba, lakini ukimuuliza kwanini, anakwambia wewe si unaona tu?
Hawezi kujenga hoja kabisa. Kwa mtu wa aina hii
huwa sipotezi muda kumsikiliza kwasababu anaongea “Mipasho tu” na natumia nguvu
kubwa kufikiria anamaanisha nini.
Lakini mtu akikosoa kwa hoja, napima uzito wa hoja
zake, kama zinazidi zangu, basi nampa kura ya ushindi na kuchukua zake na
kuacha zangu. Lakini kwa waliowengi, ni kuponda tu na kupandikiza chuki.
Leo hii Simba wanafundishwa na Patrick Phiri baada
ya Loga kuondoka. Wapo wengi walimpenda Loga na wamesikitishwa sana na kuondoka
kwake, lakini wapo waliofurahi kuondoka kwasababu hawakumpenda.
Usajili umeridhisha?: Mwenyekiti wa kamati ya usajili ya Simba sc, Zacharia Hans Poppe
Pande mbili lazima ziheshimiane vizuri. Kama
upande mmoja una hoja, wewe unayepinga weka zako mezani, tuone nani anashinda.
Siamini kama kila mtu anaweza kuwa mchambuzi mzuri wa hoja, lakini hutakiwi
kushambulia kama huwezi kujenga hoja yako.
Ya Loga yameshapita, yanayoendelea ni ya Patrick
Phiri. Kinachosubiriwa kwa sasa ni kuona nini Mzambia huyu ataifanyia Simba.
Afanikiwe asifanikiwe, ndio mpira. Ndio maana Jose
Mourinho aliyefanya makubwa na Chelsea miaka ya 2006 na kuendelea alishindwa
kubeba kombe la Ligi kuu msimu uliopita. Tena alimaliza mikono mitupu.
Phiri kubeba ubingwa bila kufungwa mwaka 2009 sio
kigezo cha kumpa asilimia 100 za kuwapa ubingwa msimu ujao. Mambo yanaweza kuwa
mazuri au mabaya. Soka huwa liko hivyo.
Kinachotakiwa ni maandalizi ya kupokea matokeo
yoyote. Najua zipo jitihada zinazofanywa ili Phiri afanikiwe, lakini kama
atashindwa kufikia malengo, kuna mambo ya msingi yatatakiwa kufanyika.
Moja wapo ni kubaini makosa yalikuwa wapi na
kuyafanyia kazi ili ajipange upya kwa msimu mwingine.
Atabebwa tena?: Patrick Phiri aliwapa ubingwa Simba mwaka 2009 bila kufungwa mechi yoyote
Ligi ya 2009 sio hii ya 2014/2015. Miaka ya nyuma
kuwa kocha wa Simba au Yanga tu, ni kura tosha ya kutwaa ubingwa. Lakini sahizi
kuna Azam fc, Mbeya City, Kagera Sugar ambao wanatoa ushindani mkubwa mno.
Kwahiyo Phiri ana kazi ngumu zaidi ya 2009 na ndio
maana nasema kuna haja ya kujiandaa kwa matokeo yoyote yale. Utamaduni ni mmoja
duniani kote, timu kubwa ina presha sana, suala la kupewa muda halivumiliki, na
ndio maana Manchester United walifanya maamuzi ya kumtoa David Moyes haraka, pia
Tata Martino kwa Barca na wengine wengi.
Lakini Man United na Barca haziwezi kuwa Simba.
Pale unawakuta wachezaji wazuri (vijana kwa ‘mafaza’) na hela za kusajili
unayemtaka zipo, lakini simba haijawa na uwezo huo. Hata mfumo wake wa kupata
wachezaji una matatizo. Kwasababu hiyo nashauri Phiri kuaminiwa na kupewa muda
mrefu.
Kuna kitu cha ziada nimekiona kwa Patrick Phiri
katika kambi yake ya mazoezi uwanja wa Chuoni Chukwani mjini Zanzibar.
Kila baada ya mazoezi, waandishi hupenda kumuuliza
Phiri, na kwa bahati mbaya maswali ni yale yale, unazungumziaje msimu ujao? Nini
wana Simba watarajie?
Mkali sana kwa wachezaji: Zdravko Logarusic alitumuliwa Simba na nafasi yake kutua mikononi mwa Phiri
Phiri amekuwa akijibu swali hilo kwa namna moja
akisema anajipanga kuwapa ubingwa Simba na kurudisha heshima iliyopotea. Kocha
huyu anawapa matumaini makubwa wana Simba kutokana na historia yake.
Lakini kuna swali la msingi napenda sana kuona
watu wanauliza, unatarajia kuijenga vipi Simba A na B ili kuwa na mwendelezo wa
uchezaji mmoja katika klabu ya Simba?
Naamini kama Simba watakaa na Phiri na kuandaa programu
nzuri ya soka la vijana watafika mbali. Tatizo la msingi la klabu ya Simba au
Yanga sio kukosa wachezaji wazuri, bali ni kukosa muendelezo wa soka la vijana.
Hivi inawezekanaje mchezaji akawa na miaka 16,17,
19 katika kikosi cha Simba B, halafu akapandishwa kikosi A na ndani ya msimu
mmoja humuoni tena? Naamini kuna tatizo linalotakiwa kutatuliwa.
Lazima utengenezwe mfumo sahihi wa kutunza na
kuendeleza soka la vijana, kama kijana amevurunda akiwa na kikosi A basi anatakiwa
kurudi tena kikosi B na sio kumuacha aondoke zake kwasababu umesajili wengine.
Jambo nililolifurahia kwa Phiri ni namna
alivyoweza kuunganisha nguvu ya pamoja kwa wachezaji. Anaonekana ni mlezi na
kocha. Wachezaji wamekuwa watulivu wakati wa mazoezi, wanamiliki mipira,
wanakaba vizuri na kushambulia.
Utulivu umerejea?. Ndiyo, Kwanini? Sababu rahisi
tu, wachezaji wamepata kocha mwenye kujua utamaduni wa soka la Simba na Afrika
kwa ujumla.
Kinachowafanya makocha wa kizungu washindwe
kufanikiwa Tanzania ni pamoja na kuleta ‘U-ulaya’ Afrika. Soka la Afrika lina
matatizo mengi hasa mfumo wa uendeshaji na aina ya wachezaji waliopo.
Wengine hawataonekana msimu ujao: Moja ya kikosi cha Simba msimu uliopita
Aina ya wachezaji wanaopatikana sio kama Ulaya.
Kuna akademi ngapi za kisasa Tanzania? Ni chache sana tena ambazo sio za
kisasa. Ukisema nahitaji wachezaji kutoka akademi za soka tu, utawapata wapi?
Ndio maana ukiangalia wachezaji wengi ni walewale,
kwasababu hakuna muendelezo wa kuwapata. Leo hii mchezaji hana misingi ya mpira
kabisa.
Kocha anafanya kazi ya kumfundisha mambo ambayo
alitakiwa kujifunza akiwa akademi wakati ana miaka 13,14, 15 au 16.
Lakini kwa wenzetu, mchezaji wa timu kubwa
anafundishwa mbinu na ufundi wa kupata matokeo na kuujenga mwili kimazoezi na
sio namna ya kupiga pasi au kupokea mpira.
Wanajua tangu
wakiwa wadogo, mazoezi ya koni wanayajua toka wakiwa wadogo, lakini kuna
wachezaji wa Bongo hata ukiwaambia wazunguke koni wanachemsha, hawajui
wafanyeje mpaka upate muda wa kuwaelekeza.
Akija kocha mzungu aliyetoka Ulaya, anawaona kama ‘wendawazimu’
lakini ndio ukweli. Ndio maana nasema kuna haja ya kujadili kutengeneza mfumo,
lakini sio kila siku kulumbana juu ya makocha na viongozi wa soka.
Simba kuna mambo matatu nawashauri ili Phiri
afanikiwe. Moja ni kumpa muda na kumuamini. Mwacheni afanye kazi yake, wekeni
mipaka ya utawala na benchi la ufundi.
Simba na Yanga nani ataibuka mbabe msimu ujao?
Fanyeni kutekeleza mahitaji yake na msisajili kwa
kushindana na upande wa pili. Kama Phiri ataachwa huru asimilia 100, nina
uhakika atafanikiwa kwasababu ana faida ya kulijulia Simba na soka la Afrika.
Pili, utawala lazima utambue malengo na ndoto za
wana Simba. Rais Aveva lazima uwe na jukumu la kuwa na mpango mkatati wa kuendeleza
timu na kuutekeleza kama timu na sio kama Rais.
Kuna vitu huwa naamini. Wapo watu wanaingia katika
soka kutafuta umaarufu na sio kuendeleza soka. Inawezekanaje kiongozi kila siku
unasikika kwenye vyombo vya habari ukiongea mipasho kwa wenzako na kuendeleza “Mabifu”?
Watu wa mipango sio wazungumzaji sana. Kama
unatekeleza mambo ya msingi na kufanikisha, kitakachojadiliwa ni mafanikio yake
na hatimaye utapata umaarufu.
Kuna faida gani kubishana na kiongozi mwenzako
kwenye gazeti? Leo hii ukifanikiwa kujenga uwanja wa Simba na kujengewe sanamu
uwanjani hapo, huoni kama ina maana kuliko kukaa kupashana na mtu kwenye vyombo
vya habari? Utawala wa Simba, fanyeni mambo ya kiutawala kwa weledi,
mtaibadilisha timu.
Tatu, wachezaji lazima waachwe wafanye kazi yao. Ni
faida kubwa kumuacha mchezaji acheze mpira vile anavyofikiria.
Sio unakwenda uwanjani na kuona Joseph Owino
anapiga chenga eneo la goli la Simba na kumrudishia kipa Ivo Mapunda, halafu
unalipuka kwa kelele, kocha toa huyooooo! Atatufungisha, piga mpira mbele bwana
wewe! Unadhani Owino hajui kama kuna kupiga mpira mbele ua kufungisha?
Hiyo ni sehemu ya mpira. Kama haoni mtu wa kuanza
naye kwanini asipige chenga wakati wenzake wanafungua?, wachezaji wanajua
wanachokifanya, lakini kwa vile wengi wanajua mpira wa mdomoni, wanaishia
kuzomea tu na kushinikiza mchezaji fulani aachwe.
Cha msingi ni kuwaamini wachezaji wenu na kuwapa
nafasi ya kuonesha uwezo wao na sio kuwapa presha kwa kutaka wacheze mtakavyo
ninyi.
Kama wanakosea unawaacha wajisahihishe. Mbona Iker
Casillas alivurunda kombe la dunia, lakini Carlo Anacelotti ameendelea
kumtumia.
Makipa wangapi wanafungisha?, mabeki wangapi wanakosea?,
washambuliaji wangapi wanakosa magoli duniani? Au Tanzania tu ndio hakuna
makosa ya kimpira, basi ni ajabu.
Kwanini akifungisha mtu asemwe kuuza mechi? Simba
waacheni wachezaji wafanye kazi yao kwa misingi ya mtaalamu Patrick Phiri.
Sina masilahi na mtu yeyote, nina masilahi na
kubadili mfumo wa soka letu.
Kila la kheri Simba na kocha mpya mwenye heshima
ndani ya klabu yenu, Mzambia, ‘Chief’ Patrick Phiri.
0 maoni:
Post a Comment