Tuesday, June 10, 2014

Fainali za Kombe la Dunia zinazoanza Alhamisi Juni 12, Afrika inawakilishwa na Nchi 5.
Zipo Ghana, Nigeria, Ivory Coast, Cameroon na Algeria na kila Mwafrika angependa kuona Timu hizi zikivunja ule mwiko wa kukwama Robo Fainali na kuziona zikitinga kwa mara ya kwanza Nusu Fainali za Kombe la Dunia.

Mwaka 2010, huko Afrika Kusini, Ghana nusura watinge Nusu Fainali kama si ‘ushenzi’ wa Straika wa Liverpool, Luis Suarez, ambae alidaka Mpira Golini na kuinyima Ghana Bao la ushindi la wazi la Dakika ya mwishoni.
Mara nyingine pekee ambapo Afrika nusura itinge Nusu Fainali ni wakati Cameroon ilipoikaba England kwenye Robo Fainali na Gemu kwenda Dakika za Nyongeza 30 huko Italy Mwaka 1990 na kisha Senegal kutolewa kiume kwenye Robo Fainali za Kombe la Dunia la Mwaka 2002. 
Je huko Brazil nani ana nafasi bora?
Ghana na Nigeria zinatinga huko Brazil zikiwa na Makocha wenye Asili za Nchi zao ambao wanataka kuweka historia ya kuwa Makocha wa kwanza Waafrika kuzivusha Nchi zao hatua ya Makundi.
Ghana wanae Kwesi Appiah na Nigeria ni Stephen Keshi.
Ivory Coast, Algeria na Cameroon zote zina Makocha wageni.


Nigeria
Nigeria wapo Kundi F na wataanza na Iran na wana Kikosi kilichosheheni wazoefu na vipajikuanzia Kipa Vincent Enyeama hadi Sentafowadi Emmanuel Emenike anaechezea Fenerbahce ya Turkey.
Kiungo yupo John Obi Mikel wa Chelsea ambae Kocha Keshi anamtaka ashambulie zaidi badala ya kuwa nyuma kama anavyocheza Chelsea.

Ghana
Ghana wapo Kundi G na wataanza na USA ambayo waliibwaga Raundi ya Mtoano ya Timu 16 huko Afrika Kusini kwenye Fainali za Kombe la Dunia za Mwaka 2010.

Baada ya USA, Ghana wana kimbembe dhidi ya Germany na Portugal ya Mchezaji Bora Duniani, Cristiano Ronaldo.
Lakini Ghana ni Timu pekee Afrika yenye Vipaji asilia na safari hii wapo kina Asamoah Gyan, Ayew, Mtoto wa Abedi Pele anaechezea Marseille, KwadwoAsamoah wa Juventus, Kevin-Prince Boateng wa Schalke 04 na Mkongwe Michael Essien.

Ivory Coast

Ivory Coast ndio Timu iliyojaza Majina makubwa kupita yeyote Afrika na wapo chini ya Mfaransa Sabri Lamouchi mwenye asili ya Tunisia.
Wapo Ndugu wawili, Yaya Toure na Kolo Toure, wapo Gervinho, Didier Zokora, Winga wa zamani wa Chelsea, Salomon Kalou, Wilfried Bony na pia yupo Didier Drogba.
Majina yote hayo na mengine mengi yanacheza Klabu kubwa Ulaya.
Huko Brazil, Kundi la Ivory Coast lina Japan, Colombia na Greece.

Cameroon
Cameroon wapo Kundi A pamoja na Wenyeji Brazil, Croatia na Mexico.
Wakongwe hao wa Afrika wako chini ya Kocha wa Germany Volker Finke na wameelekea huko Brazil baada ya Mgomo wa Masaa 12 Wachezaji walipogoma wakipinga Bonasi ndogo.
Ingawa wana Kikosi cha wazoefu kina Samel Eto’o, Kipa Charles Itandje, Alex Song na wengineo, matayarisho yao yameleta shaka kubwa.

Algeria

Wako chini ya Kocha kutoka Bosnia, Vahid Halilhodzic, na Wachezaji wao karibu wote ni wale wenye makazi huko Ulaya hasa France.
Kwa sasa mwenye Jina kubwa linalovuma kwenye Kikosi chao ni Kiungo wa Valencia Sofiane Fegouhli.

Wachezaji-Nani Nyota mpya?

Mbali ya Yaya Toure, ambae ndie Mchezaji Bora Afrika kwa Miaka Mitatu iliyopita na Didier Drogba na Samuel Eto’o ambao nao wamezoa Tuzo hiyo mara 5 kati yao katika Miaka 7 iliyopita, nani mpya anaweza kuibuka Nyota Mpya wa Afrika huko Brazil?

0 maoni:

Post a Comment

waliotembelea blog