Tuesday, May 6, 2014


Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limeazimia kuanzisha Mfuko wa Maendeleo ya Mpira wa Miguu Tanzania (TFF Development Trust Fund).
Uamuzi wa kuanzisha mfuko huo umepitishwa katika kikao cha Kamati ya Utendaji ya TFF iliyokutana Mei 3 mwaka huu jijini Dar es Salaam ambapo madhumuni yake ni kutafuta vyanzo vya rasilimali za kuendeleza programu za mpira wa miguu Tanzania.
Mfuko huo utakaokuwa chini ya uenyekiti wa Rais aliyepita wa TFF, Leodegar Tenga utatafuta rasilimali za kuendeshea michuano ya Taifa na kimataifa ya wavulana na wasichana kwa vijana wenye umri chini ya miaka 13, 15, 17 na 19.
Pia kuendeleza maeneo ya ardhi kote Tanzania ambayo ni mali ya TFF kwa kujenga vituo vya michezo (sports centres), kutafuta rasilimali za kutoa mafunzo kwa makocha, marefa, madaktari wa tiba ya michezo na viongozi (administrators).

Majukumu mengine ya mfuko huo ni kuagiza na kusambaza vifaa vya michezo hasa kwa watoto wadogo (grassroots) na vijana.

Mfuko huo utazinduliwa Oktoba 8 mwaka huu ambayo ni siku ya kilele cha Tanzania kutimiza miaka 50 ya uanachama wake katika Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA).

Mbali ya Tenga, wajumbe wengine wanaounda bodi ya mfuko huo ni Mwenyekiti wa zamani wa Simba, Ayoub Chamshama, Katibu Mkuu wa zamani wa TFF, Fredrick Mwakalebela, Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Michezo ya Kubahatisha, Tarimba Abbas na Mbunge wa Viti Maalum, Zarina Madabida.

MWINYI KAZIMOTO ATUA TAIFA STARS
Kiungo mshambuliaji wa timu ya Al Markhiya ya Qatar, Mwinyi Kazimoto amewasili nchini kujiunga na kikosi cha Taifa Stars kinachojiandaa na mechi ya michuano ya Afrika dhidi ya Zimbabwe.

Kazimoto ambaye amewasili nchini jana (Mei 5 mwaka huu) anatarajia kusafiri leo (Mei 6 mwaka huu) kwenda Tukuyu mkoani Mbeya ambapo Taifa Stars imeweka kambi yake chini ya Kocha Mart Nooij kujiandaa kwa mechi hiyo.

Taifa Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager juzi (Mei 4 mwaka huu) ilicheza mechi ya kirafiki na Malawi (Flames) ikiwa ni sehemu ya maandalizi kabla ya kuikabili Zimbabwe (Mighty Warriors). Mechi hiyo dhidi ya Flames ilichezwa Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine na kumalizika kwa suluhu.

WACONGO KUCHEZESHA MECHI YA NGORONGORO HEROES
Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) limeteua waamuzi kutoka Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo (DRC) kuchezesha mechi kati ya Tanzania (Ngorongoro Heroes) na Nigeria.

Mechi ya mchujo kusaka tiketi ya kucheza Fainali za 19 za Afrika kwa vijana wenye umri chini ya miaka 20 zitakazofanyika mwakani nchini Senegal itachezwa wikiendi hii jijini Dar es Salaam.

Waamuzi hao wataongozwa na Jean-Jacques Ndala Ngambo atakayesaidiwa na Oliver Safari Kabene, Nabina Blaise Sebutu na Mupemba Ignace Nkongolo. Kamishna wa mechi hiyo namba 37 ni Poiret Antoine Ralph Danny kutoka Shelisheli.
BONIFACE WAMBURA
OFISA HABARI NA MAWASILIANO
SHIRIKISHO LA MPIRA WA MIGUU TANZANIA (TFF)

0 maoni:

Post a Comment

waliotembelea blog