Wednesday, December 18, 2013



 


  • Hata hivyo, Waingereza ni watu makini na ambao linapokuja suala kama hilo, huweza kutumia baadhi ya nguvu kulisukumiza mbali kana kwamba haliwahusu kabisa.

KAMA siku 10 zilizopita kuliibuka habari kuhusu kashfa ya upangaji matokeo katika soka la England.
Mambo haya yamepokewa kwa mtikisiko na hisia tofauti kwa sababu yanaweza kuathiri ile hadhi ya soka la hapa, hasa ikizingatiwa kwamba England ndiyo nchi yenye ligi maarufu zaidi duniani.
Hata hivyo, Waingereza ni watu makini na ambao linapokuja suala kama hilo, huweza kutumia baadhi ya nguvu kulisukumiza mbali kana kwamba haliwahusu kabisa.
Hata katika hili, wengi niliozungumza nao wamesema kwamba kwanza si kitu kipya katika historia ya soka, lakini wengine wanakazia kwamba wanaohusishwa na kashfa hiyo ni wachache hivyo washughulikiwe kikamilifu. Kuna jamaa mmoja ambaye amepata kufanya kazi Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa) ambaye anasema haya ni mambo sawa na ndoto za mchana na yapuuzwe tu.
Katika madai yaliyotolewa wiki iliyopita, baadhi ya wachezaji (bahati mbaya ni Waafrika au wana asili ya Afrika na Singapore), wanadai kwamba walizoea kupanga matokeo kwa namna ya kuziathiri timu zao.
Mnigeria mmoja, Sam Sodje, anasema alikuwa akitengeneza mambo kwa kupewa fedha hadi Pauni 70,000 ili acheze faulo mpaka aonyeshwe kadi za njano au hata nyekundu.
Lakini pia aliwashawishi wachezaji wengine ndani na nje ya timu yake akiwa wakala wa rushwa na upangaji matokeo kisha wakapata kulipwa, yote hayo aliyafanya katika soka la England.
Hili ni jambo linalowaumiza sana watu wa hapa, hivyo kuna wanaoshauri wote waliohusika wafungiwe maisha.
Haya mambo husanuka katika hali ya ajabu, kwa vile awali huwa ni siri kubwa kati ya ‘wakala’ na mchezaji anayefikiwa kwa ajili ya kuisaliti timu yake ili ifungwe.
Hata hivyo, kwa kuwa wanasema za mwizi ni 40, mazungumzo yangu na baadhi ya wadau yanaonesha kwamba siri hii hushindikana kufichwa kwa sababu mbalimbali.
Moja ni utoto au ulevi wa wachezaji wanaohusishwa na kashfa hizo, ambapo hushindwa kuhifadhi vifuani mwao siri husika wanapokuwa kwenye maeneo ya starehe.
Lakini pili, kwa hapa England suala la kamari ni kubwa japo mizizi yake mikubwa ipo kule barani Asia.
0
Share

0 maoni:

Post a Comment

waliotembelea blog