Thursday, December 17, 2015



SHIRIKISHO la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limefanya marekebisho ya kanuni za usajili ambapo sasa mchezaji ambaye usajili wake utakuwa umepita kwenye mfumo wa mtandao wa Transfer Matching System (TMS) atapewa leseni na kuitumikia moja kwa moja timu yake mpya.

TFF itatoa leseni ya usajili wa mchezaji ambaye amethibitishwa kupitia mtandao wa TMS baada ya kuwepo nyaraka zote; mkataba uliomalizika, barua ya kuvunja mkataba, barua ya kuachwa (release letter), mkataba mpya na uthibitisho wa makubaliano kati ya klabu zinazohusika.

Licha ya mchezaji kupata leseni, Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji bado itakuwa na mamlaka ya kushughulia upungufu, malalamiko ya kiusajili, pingamizi na uhalali wa kimkataba kati ya pande mbili (mchezaji na klabu).

Wachezaji wote wa kigeni waliosajiliwa kwa ajili ya kucheza Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) wanapaswa kulipiwa dola za kimarekani U$ 2,000 kwa kila mmoja kabla ya kupatiwa leseni na kuanza kuzitumikia klabu zao katika michuano ya Ligi Kuu na Kombe la Shirikisho.

Pia TFF kupitia kamati ya sheria na hadhi za wachezaji inaweza kumruhusu kwa kipindi maalum mchezaji mwenye dosari acheze kwa leseni ya muda (provisional license) hadi dosari hizo kati ya klabu na klabu zitakapomalizwa. Iwapo dosari hizo hazitakuwa zimemalizwa, mchezaji anaweza kuzuiwa kucheza na klabu husika kuadhibiwa.


Timu zote za Ligi Kuu, Ligi Daraja la Kwanza na Ligi Daraja la Pili zinatakiwa kufuatilia TFF kujua wachezaji ambao hawana pingamizi na leseni za wachezaji waliopitishwa wanaweza kuanza kutumika kuanzia kesho tarehe 18/12/2015 na kwenye michezo ya kombe la Shirikisho (FA Cup) kama hawakuwa wamecheza raundi ya kwanza kwenye vilabu vya zamani.

0 maoni:

Post a Comment

waliotembelea blog