Friday, December 18, 2015




Wanamuziki nyota wa bongo fleva nchini, Estelina Peter Sanga maarufu kwa jina la Linah Sanga na Feza Kessy  ijumaa watapanda jukwaa moja na nyota kibao wa Nigeria katika tamasha kubwa la mwaka la muziki lijulikanalo kwa jina la Soundcity Urban Festival.

Tamasha hilo pia litawashirikisha wasanii nyota wa Nigeria kama, Davido, Kiss Daniel, Iyanya na  Olamide. Katika orodha hiyo wapo wasanii nyota wengine kama  Victoria Kimani, Runtown, Sound Sultan, Lil Kesh, Ycee, Sean Tizzle na Phyno.

Wanamuziki hao waliondoka nchini Jumatano usiku chini ya Doreen Noni ambaye ni Mkurugenzi wa kampuni mpya ya kusimamia wanamuziki nchini, Panamusiq Limited.



Doreen alisema kuwa kampuni yao ndiyo iliyowawezesha wanamuziki hao kuweka historia kwa kuwa wanamuziki wa kwanza nchini kushiriki katika tamasha hilo kubwa la muziki litakalofanyika mjini Lagos.

 Alisema kuwa Panamusiq Limited imepanua wigo wa shughuli zake na kwa sasa inafanya kazi na kampuni nyingi maarufu duniani zinazojishughulisha na masuala ya muziki.

“Tumejiandaa kufanya kweli katika tamasha hilo, Linah na Feza walikuwa katika mazoezi makali ya kuimba, kucheza hasa kwa kutawala jukwaa, lengo ni kuacha historia katika tamasha hilo,” alisema Doreen.

 Doreen alisema kuwa  kampuni yao yenye maskani yake Kinondoni jijini, imepania kuwatambulisha wasanii kimataifa pamoja na kuwaongezea kipato kutokana na kazi zao.

“Linah na Feza ni miongoni tu mwa wasanii ambao wapo chini ya kampuni yetu ambayo lengo lake kubwa ni kuwaendeleza na kufaidika kupitia kazi zao, najua kuna wanamuziki wengi sana hapa nchini, wachache sana ndiyo wapo kimataifa zaidi, sisi tunataka wafikie mamia na kupanua soko lao,” alisema Doreen.

0 maoni:

Post a Comment

waliotembelea blog