Friday, October 23, 2015



JUMAPILI ya Oktoba 25, 2015, Tanzania inafanya Uchaguzi Mkuu wa madiwani, wabunge pamoja na kumpata Rais wa Awamu ya Tano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Uchaguzi ni nini? Zipo tafsiri mbalimbali lakini mojawapo na iliyo wazi ni kwamba, hii ni njia ya kidemokrasia inayotumiwa na watu katika kuchagua viongozi wa kuwaongoza kwa kipindi fulani kwa mujibu wa Katiba au utaratibu waliojiwekea wenyewe.
Huu ni Uchaguzi Mkuu wa Tano kufanyika tangu mfumo wa vyama vingi ulipoanza tena mwaka 1992, lakini ni wa 11 tangu Tanganyika na Zanzibar zilipoungana mwaka 1964.
Uchaguzi wa mwaka huu una umuhimu wa kipekee kwa sababu kadha wa kadha, mojawapo ikiwa umri wa miaka 23 tangu mfumo wa vyama vingi ulipoanza.
Huu ni umri mkubwa, na kwa hakika vijana wengi waliojitokeza kujiandikisha safari hii ni wenye umri wa kati ya miaka 18-35, ikimaanisha kwamba wengi wao walizaliwa kuanzia mwaka 1992. Hawa wanatengeneza asilimia 57 ya wapigakura wote.
Umuhimu mwingine ni kwamba, kulinganisha na uchaguzi wa kwanza wa vyama vingi mwaka 1995, safari hii demokrasia imekua na kupanuka kiasi cha kushuhudia wapigakura 22.75 milioni, idadi ambayo ni kubwa zaidi kuwahi kutokea nchini tangu tupate Uhuru.
Kwa upande mwingine, hamasa imeongezeka, upinzani umeimarika zaidi na uhuru wa habari umepanuka ukiwamo ukuaji wa sekta ya habari na mawasiliano, hususan mitandao ya kijamii.
Haya yote yanatokea kutokana na kuwapo kwa amani na utulivu, sifa ambazo zimeendelea kuitambulisha vyema Tanzania hata katika jumuiya za kimataifa.
Uchaguzi Mkuu ni gharama kubwa kifedha, rasilimali watu na muda, na kama mambo yatakwenda mrama maana yake nchi itakuwa imeingia hasara kwa kupoteza fedha, lakini pia itaingia kwenye machafuko ambayo yatatowesha amani iliyodumu kwa miaka mingi.

0 maoni:

Post a Comment

waliotembelea blog