Tuesday, August 13, 2013


NIANZE kwa kumshukuru Mungu kwa kuweza kutupa uhai na tumuombe atuzidishie moyo wa upendo ili tuwe na amani katika nchi zote hasa za  Afrika Mashariki.
Hakuna shaka yoyote nikisema kwamba uhai na ustawi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) upo mashakani kutokana na viongozi wa nchi hizo kuonesha kutoshikamana.
Inanikumbusha mwaka 1977, EAC iliposambaratika na kutokana na itikadi za kisiasa licha ya kuasisiwa na Marais, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere (Tanzania), Jomo Kenyatta (Kenya) na Dk. Milton Obote (Uganda)  ingawa safari hii suala la itikadi zinazokinzana haliwezi tena kuwa sababu au chanzo cha kuparaganyika kwa jumuiya.
Kwa waliokuwa vijana au watu wazima zama hizo, wanakumbuka jinsi EAC ya wakati ule ilivyovunjika na kuiacha kila nchi kati ya Tanzania, Kenya na Uganda ikichukua mali, madeni ya jumuiya hiyo na kila moja na msimamo wake, ikiendesha pia mambo yake kwa mgawanyo wa mali ambao haukuwa wa haki.
Lakini baadaye marais wa nchi hizo, Benjamin Mkapa (Tanzania), Daniel arap Moi (Kenya) na Yoweri Museveni (Uganda) wakaanzisha juhudi mpya zikawezesha kurejea na kuzaliwa upya kwa EAC  yenye makazi yake Arusha, mahali ambako zimewekezwa fedha lukuki kujenga makao makuu mapya, ingawa kwa sasa jumuiya hiyo inayumba.
EAC ya sasa inayumba licha ya kuongezwa nguvu kwa kuzijumuisha nchi za Rwanda na Burundi kama wanachama wake wapya, jumuiya ina nyufa kubwa ambazo kwa mtazamo wangu zinaashiria kuanguka au kuporomoka siku si nyingi zijazo.
Baadhi ya watu walidhani kwamba EAC yetu ya sasa ingekuwa jumuiya moja kubwa yenye nguvu kibiashara, kisiasa, lakini ndoto hizo zimekwisha na tayari (EAC) imegawanyika katika makundi.
Hakuna shaka kwamba makundi hayo yanatokana na mitazamo ya kimasilahi zaidi ya viongozi wakuu wa nchi tatu,  hasa Rwanda, Kenya na Uganda, kwa kweli yanaiacha EAC ya sasa katika hatari ya kufa kabla ya kutimiza malengo yake.
Ni bahati nzuri kwamba Burundi, nchi ambayo imekuwa katika mizozo mingi ya ndani, vita ya wenyewe kwa wenyewe, haina upande katika mzozo huu wa sasa wa EAC.
Kwa mtazamo wa kawaida mgogoro unaweza kuonekana kuwa ni kati ya Rais Jakaya Kikwete na Rais wa Rwanda, Paul Kagame huku wengine wakiwa ni mashabiki na huenda hata Kenya ya Rais Uhuru Kenyatta na Uganda ya Yoweri Museveni zinaiona Tanzania kama tishio kwa masilahi yao.
 Hakuna shaka kwamba matarajio ya wengi katika jumuiya hiyo ni kuifikiria Tanzania kama eneo la kuingia kiholela, kujichotea mali, ardhi, ajira kama wapendavyo kupitia EAC lakini sasa wanaona kuna ugumu, hivyo kuanzisha chokochoko.
Uganda kwa mfano, ni nchi  ambayo siku zote imekuwa ikifumbia macho magendo ya kahawa, maharage, ndizi kutoka Kagera kupitia njia za panya  mpakani.
Huenda nayo inaona kwamba biashara hii kuwa si endelevu kama ilivyo pengine kwa kufanya biashara au ushirikiano  mzuri zaidi na Kenya kwa njia ya barabara na reli.
Tuliwahi kushuhudia Museveni akimualika Kenyatta na Kagame nchini mwake na Kikwete hawakumualika, tena walisema walikuwa wanazungumzia maendeleo ya Afrika Mashariki!
Hii yote inatokana na Rais Kikwete, katika kikao cha mwaka cha Umoja wa Afrika (AU), kilichofanyika mwanzoni mwa Juni, mwaka huu, mjini Addis Ababa Ethiopia kutoa ushauri kwenye Kamisheni ya Ulinzi na Usalama ya umoja huo, kwamba ili kutafuta suluhisho la kudumu la hali ya kiusalama katika nchi za Maziwa Makuu, upo umuhimu kwa Marais Kagame, Museveni na Joseph Kabila wa DRC kuzungumza na makundi ya waasi wanayopambana nayo katika nchi zao.
Makundi hayo ya waasi ni pamoja na Democratic Forces for the Liberation of Rwanda (FDLR), kundi ambalo Rais Kagame amekuwa akisisitiza linaundwa na Wanyarwanda waliokimbilia DRC mwaka 1994, baada ya kutekeleza mauaji ya kimbari, wanaojulikana kwa jina la Interahamwe. Mengine ni Allied Democratic Force (ADF) kwa upande wa Uganda na M23 kwa Rais Kabila wa DRC.
Ushauri huo haikuwa amri, kinyume chake, Rais Kagame aliukataa kwa kutoa matusi na kejeli kwa mwenzake!
Marais hao hawatakuwa viongozi wa kwanza kupewa ushauri na Rais Kikwete kwani itakumbukwa alikuwa mmoja wa viongozi walioshiriki kumshauri Rais Mwai Kibaki wa Kenya akubali kuzungumza na mpinzani wake, Raila Odinga baada ya Uchaguzi Mkuu wa 2007 uliomalizika kwa vurugu na uvunjifu wa amani na akakubali.
Inawezekana Kagame ana chuki ya muda mrefu dhidi ya Tanzania kwani hakufurahishwa hata kidogo na hatua ya Tanzania kushirikiana na nchi za Afrika Kusini, Malawi na Msumbiji, kupeleka majeshi ya kulinda amani nchini DRC, eneo lenye madini mengi na Rwanda wapo huko kwa kisingizio cha kuwasaka FDLR.
Nimwambie Rais Kagame kwamba hakuwa na sababu ya kumtukana Rais Kikwete kwani angeweza kutofuata ushauri aliopewa na kila kitu kikaishia hapo.

0 maoni:

Post a Comment

waliotembelea blog