Tuesday, August 6, 2013


Chokochoko  zinazoendelezwa na Rais wa Rwanda, Paul Kagame (pichani) dhidi ya Rais Jakaya Kikwete zimewakasirisha baadhi ya wananchi wakiwemo askari wa Tanzania na wakadai kuwa kiongozi huyo wa Rwanda atakiona cha moto akianza uchokozi.

Wakizungumza na gazeti  la UWAZI  mwishoni mwa wiki iliyopita kwa sharti la kutoandikwa majina yao gazetini, baadhi ya askari walisema wanamshangaa Kagame kuitishia Tanzania wakati anajua kuwa hana ubavu wa kupigana nayo.


Askari wengi waliohojiwa, walisema Rwanda haina uzoefu wowote katika vita ya kimataifa ukilinganisha na Tanzania na Kagame akianzisha vita ni yeye atakayekufa kwa sababu vita haina macho.


“Kagame anajua kwamba Rais Kikwete si mgomvi na alimpa ushauri tu kwa kumwambia azungumze na waasi nchini mwake sasa kwa nini anaendelea kufanya chokochoko? Akianza vita itamuua. Kwa nini anamdhalilisha rais wetu?” alisema askari mmoja.

 
 Akaongeza: “Kagame amezoea vita ya wao kwa wao lakini Tanzania tumeshakwenda nchini Comoro ili kumng’oa Kanali Mohamed Bacar ambaye alikuwa aking’ang’ania madaraka katika Kisiwa cha Anjouan, tulipigana na Nduli Iddi Amin na akakimbia nchi, sembuse Kagame?” alihoji askari huyo.

Akaongeza: “Tumekwenda Msumbiji, Angola, Visiwa vya Shelisheli, Darfur na hata Lebanon, siyo kwa kuvamia bali kwa kuombwa na mataifa, hivyo Kagame aache kabisa kumkashifu rais wetu, amheshimu kama anavyoheshimiwa yeye.”

Licha ya askari, wananchi mbalimbali waliohojiwa na gazeti hili, wamemshangaa Kagame kwa kumtusi Kikwete.


“Kwangu mimi nasema ni bora tukaachana na huu mpango wa Shirikisho la Afrika Mashariki kwa sababu dalili mbaya zinaonekana hata kabla ya kuungana,” alisema Naomi Erasto, Mkazi wa Masaki, Dar.

Akaongeza kuwa Kagame  ni  lazima  atambue  kwamba  Watanzania  wapo  tayari  kuilinda  nchi  yao kwa  gharama  yoyote  na  kamwe  hawawezi  kuwa  vibaraka wa Rwanda.

Rais Kikwete alimpa ushauri Kagame wakati wa mkutano wa kujadili amani na mpango wa ulinzi nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo uliofanyika katika Makao Makuu ya AU, Addis Ababa, Ethiopia mwaka huu.

Katika ushauri huo, Rais Kikwete alisema kwamba ni vyema Rais Kagame akakaa katika meza ya mazungumzo ya amani na Rais wa Kongo, Joseph Kabila ili kumaliza tofauti zao badala ya kutumia nguvu za kijeshi.

Badala yake, Kagame akajibu: “Nimekaa kimya kwa kipindi kirefu na kwa jinsi nilivyoweza kwa sababu nilifikiri kwamba mazungumzo ya kipuuzi yaliyozungumzwa na watu wajinga yamemalizika,” alisema Rais Kagame.

Akasema ushauri huo wa Rais Kikwete ni sawa na kuwachezea Wanyarandwa mbele ya mataifa.

Kagame aliyasema hayo katika sherehe za kuhitimu mafunzo ya maofisa wa jeshi wapatao 45 katika kituo cha mafunzo huko kwao na alipowahutubia vijana, Juni 30, 2013 kwenye mkutano wao wa “Youth Konnect” uliofadhiliwa na mke wake, Janet Kagame.

Kwa mara ya kwanza, Rais Kikwete alimtolea uvivu Rais Kagame mwishoni mwa wiki iliyopita, akasema ushauri ule aliutoa kwa nia njema kabisa kwani bado anaamini kuwa kama jambo linaweza kumalizwa kwa njia ya mazungumzo, ni vyema itumike.


“Isitoshe, ushauri ule niliutoa pia kwa Serikali za Kongo na Uganda. Katika mkutano ule Rais Museveni wa Uganda aliunga mkono kauli yangu. Rais Kagame hakusema chochote pale mkutanoni.


“Kwa upande wangu sijasema lolote kuhusu Rwanda pamoja na maneno mengi ya matusi na kejeli yanayotoka kwenye vinywa vya viongozi wake dhidi yangu. Siyo kwamba siambiwi yanayosemwa au sijui kusema au sina la kusema, la hasha, sijafanya hivyo kwa sababu sioni faida yake,” alisema Kikwete
.


0 maoni:

Post a Comment

waliotembelea blog