MWIGIZAJI wa filamu Bongo, Elizabeth Michael ‘Lulu’, amezungumzia historia ya maisha yake na matukio aliyopitia katika umri wake ambao katika hali ya kawaida ni mdogo kwa mhusika kuwa gumzo kwenye jamii.
Lulu alijikuta akiwa mahabusu ya Segerea baada ya mpenzi wake Steven Kanumba kufariki akiwa naye. Wengi walishangaa na kutoamini kuwa wasanii hao walikuwa wapenzi kwani jambo hilo halikuwahi kujulikana.
Uhusiano na Kanumba
Lulu anasema yeye na marehemu walikuwa na uhusiano wa kimapenzi kwa muda mrefu, lakini moja ya makubaliano yao ilikuwa ni kuishi katika maisha ya siri hiyo. Katika hilo hataki kuzungumzia undani wa siri iliyokuwapo baina yao.
“Mapenzi yangu na Kanumba ilikuwa ni makubaliano yetu kufanya iwe siri, nadhani haikuwa na maana kwetu, mapenzi yalikuwa ya muda mrefu, lakini sitaki kuzungumzia uhusiano wetu kutokana mambo mengi yamepita,” anasema.
Msanii huyo anakiri alitamani kuhudhuria mazishi ya mpenzi wake huyo, lakini haikuwa rahisi kwani alikuwa rumande.
Anasema maisha ya mahabusu yamemjenga na kumfanya kuwa mtu tofauti. Anasema sasa anaona kuwa anao wajibu wa kutumia muda wake kupitia filamu, kuwaelimisha vijana na watu wazima kuhusiana na maisha.
Katika hilo anasema anaandaa filamu mbili ikiwamo ya ‘Mapenzi Ya Mungu’.
Anasema ‘Mapenzi Ya Mungu’ ameigiza kwa kushirikiana na Mama mzazi wa marehemu Kanumba (Flora Mtegoa).
Anasema filamu hiyo inaeleza kuhusu maisha yake alipokuwa rumande, kikubwa hapo anasema maisha ya huko yamemfanya amjue Mungu zaidi.
Lulu anasema kuwa filamu yake ambayo ipo tayari inasubiri kuzinduliwa wakati wowote ni ya ‘Foolish Age’ inayoelezea maisha yake na majanga aliyopitia.
Anaamini kuwa wakati mtu anapokuwa katika umri mdogo, anaweza kufanya mambo ya hatari ambayo si rahisi kabisa kuyabaini kwa muda huo na hata kama akionywa hawezi kuelewa.
0 maoni:
Post a Comment