Sunday, September 14, 2014


Na baraka Mbolembole, Dar es Salaam,
Salum Telela alifunga bao pekee kwa kuunganisha krosi ya mshambulizi Didier Kavumbangu na kuisaidia timu yake kupata ushindi wa bao 1-0 katika mchezo wa Ngao ya Jamii, mwaka uliopita.. Kelvin Yondan, Nadir Haroub, Saimon Msuva, ni wachezaji pekee ambao wanaweza kuanza moja kwa moja katika kikosi cha kwanza cha Mwalimu, Marcio Maximo. Mfungaji wa mwaka uliopita Telela na mlinzi wa kulia Juma Abdul ambao wote walianza katika mchezo wa ushindi mwa jana, mmoja wao atasubiri katika benchi ili kupisha utitiri wa viungo katikati ya uwanja.
Aishi Manula, Erasto Nyoni, David Mwantika, kaimu nahodha Aggrey Morris, Himid Mao Mkami, Salum Abubakary, Kipre Tchetche, Kipre Bolou wote hao walianza katika mchezo wa kichapo mwaka jana na wanataraji kuanza katika mchezo wa leo ambao utakuwa watatu mfululizo kwa kikosi chao cha Azam FC katika Ngao ya Jamii. Mabingwa hao wa ligi kuu Bara msimu uliopita, wana safu kabambe ya mashambulizi ambayo ilifunga mabao 12 katika michezo mitano ya Kagame Cup, Mwezi uliopita nchini Rwanda.
Wakati kocha wa Yanga, Maximo akitaraji kumuanzisha mshambulizi mmoja mbele, huku akitegemea safu ya kiungo kama muhimili wa timu, Joseph Omog yeye yupo tofauti , licha ya kumkosa nahodha wake John Bocco, kocha huyo raia wa Cameroon atakuwa na nafasi nzuri ya kujaribu safu yake ya ‘ washambulizi watatu wa kimataifa’. Tchetche, Mhaiti, Lieonel Saint na Mrundi, ‘ Kavu’ ambaye alifunga mabao 22 katika misimu miwili ya ligi kuu Bara akiwa na kikosi cha Yanga. Yanga watapata shinda lakini sehemu yao ya katikati ya uwan ja inatakiwa kuwa ngumu zaidi ya ilivyokuwa katika michezo minne iliyopita ya maandalizi ambayo wameshuhudia timu yao ikifunga mabao matano tu.
AZam ni lazima watafunga, wanaweza kufunga hata mabao mawili kwa sabu safu yao ya mashambulizi ina wafungaji wa uhakika. Kama Leonel ataachana na tabia yake ya kutotoa ushirikiano na kujiona staa zaidi ya wenzake itaendelea Azam itaanguka na wanaweza kupoteza mchezo. Safu ya ulinzi ya Yanga ndiyo ile inayotumika katika timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars, golikipa Deogratius Munish ana nafasi kubwa ya kuanza mchezo huo lakini nafasi hiyo inaweza kuangukia kwa ‘ mwalimu wa uwanjani’ Juma Kaseja,  nahodha Nadir, Kelvin a Oscar Joshua katika upande wa kushoto ni nafasi nne ambazo zinapangika kwa urahisi.
Maximo  kama ilivyo kwa Omog naye atakuwa akikuna kichwa, ni mlinzi gani sahihi wa kulia ambaye anatakiwa kumpanga katika mfumo wake na kufanya vizuri. Abdul au Telela? Ogog atakuwa akitafakari nafasi hasa ya kumpanga Nyoni mchezaji ambaye anaingia katika mifumo yote. Nani atamchezesha nafasi ya ulinzi wa kushoto? Ni Nyoni, Said Mourad au kinda Gadiel Michael ambaye alifanya vizuri katika michuano ya Kagame?. Makocha wote wanapasuka vichwa, hiyo ni kutokana na wachezaji wa timu pinzani jinsi wanavyocheza na u-fit wao walionao sasa.
Maximo amekuwa akitumia mfumo wa  4-5-1 ambao huwapanga viungo watano, Hasan Dilunga upande wa kulia,  Mbuyu kama kiungo wa kwanza wa ulinzi-namba 6,  Andrey Coutinho kama kiungo wa mashambulizi akitokea upande wa kushoto, Niyonzima kama kiungo ‘ mchezesha timu mkuu’ –namba 8, Msuva amekuwa akitumika kama mshambulizi wa pili. Kwa nini imekuwa hivyo? Mbuyu ni mkabaji hasa na mchezaji anayeanzisha pasi nzuri kwa viungo wa mbele. Dilunga ni mchezaji mwenye nguvu katika miguu na mwili wake , ni mwepesi hivyom ni rahisi kwake kucheza kama kiungo wa kulia, wakati mwingine upande wa kushoto, kama ataendelea kupiga pasi zinazofika bila shaka ni chaguo ambao Maximo hatajutia. Vipi kuhusu nafasi ya Mrisho Ngassa? Maximo anaweza kumpanga Nassa kama mshambulizi wa pili nyuma ya GEilson Santos ‘ Jaja’ na ikiwa hivyo itamaanisha Dilunga arudi katika benchi na Msuva acheze kama kiungo wa kulia. Itafaa zaidi , Ngassa akicheza, kwa sababu viungo wa Azam ni ‘ wagumu na hawachoki’ mapema. Himid, Salum, na Bolou itakuwa safu nzuri ya kiungo kwa upande wa kikosi cha Omog, lakini anaweza kumtumia Nyoni katika eneo hilo ikiwa atachezesha timu yake katika mfumo wa 4-4-2.
Azam wana safu nzuri ya ulinzi ambayo kwa kiasi kikubwa ilichangia mafanikio ya timu hiyo katika ligi kuu Bara msimu uliopita waliporuhusu mabao 15 katika michezo 26. Morris, Mwantika ni chaguo zuri la kwanza katika safu ya ulinzi wa kati. Jaja atafunga katika mchezo wa leo ikiwa viungo wake watamiliki mchezo. Shomari Kapombe atakutana na kiungo mwenye maarifa, Couinho na upande wa kulia wa Azam umekuwa na mchezo usioridhisha sana kwani upande huo upitika kiurahisi, ili kuziba nafasi ya Yanga kutumia upande wao wa kushoto Omog ni lazima amuanzishe nje mshambulizi wake mmoja ili kumpatia nafasi Nyoni katika eneo la kiungo kuwasaidia, Himid, Salum na Bolou.
Said Mourad atakuwa na nafasi finyu ya kuanza katika safu ya ulinzi wa kati, lakini ili kuleta usawa na nguvu zaidi katika ngome, Omog anaweza kupata faida kubwa akimpanga mchezaji huyo katika eneo la ulinzi wa kushoto.  Ni mechi ngumu lakini inaweza kuwa ya mabao mengi, 3-2, 2-1 au 3-1 ni matokeo ambayo yanaweza kutokea. Ipi timu bora zaidi katika mchezo wa leo? Yanga? Ubora wao uko wapi?
Azam ikiimaliza sehemu ya kiungo ya Yanga watashinda, ila watafungwa wakiruhusu vipaji vya Yanga kutawala katikati ya uwanja. Kavumbagu atafunga, Jaja atafunga ila ningempanga Telela katika eneo la kiungo la Yanga ili kuwamudu Azam FC ‘ mwanzo-mwisho’. Ningempanga Nyoni katika kiungo na Mourad katika safu ya beki tatu ili kupunguza krosi za Yanga. Yanga ina nafasi ya kushinda kwa mara nyingine….AZam FC ililazwa na Simba SC kwa mabao 3-2, 2012, wakapoteza mbele ya Yanga kwa bao 1-0, 2013, 2014 itakuwaje, Ngao ya Jamii si bahati yao?

0 maoni:

Post a Comment

waliotembelea blog