DIEGO
ARMANDO MARADONA, Lejendari wa Argentina, amesema Nchi yao inacheza
chini ya kiwango, wanamtegemea sana Lionel Messi na lazima waongeze
juhudi ikiwa watataka kuifunga Belgium kwenye Robo Fainali ya Kombe la
Dunia ambayo watakutana Jumamosi Usiku.
Maradona amesema: “Bado hatujaanza!
Lazima watambue wazi, waweke vichwani mwao, si kumtegemea Messi tu.
Labda anaweza kufunga Bao safi…lakini kama hakuweza, wasimrukie Kijana
huyu na kumfanya ndie mwenye hatia ya maafa ya Argentina!”
Maradona, ambae ndie alikuwa Kocha wa
Argentina kwenye Fainali za Kombe la Dunia za Mwaka 2010 huko Afrika
Kusini walikotolewa Robo fainali, alikuwa akihojiwa na TV ya Venezuela
mara baada ya Argentina kuitoa kwa mbinde Switzerland kwa Bao 1-0 la
mwishoni la Dakika za Nyongeza 30 lililofungwa na Angel Di Maria baada
kazi njema ya Messi.
Akizungumzia Mechi hiyo, Maradona
alisema: “Mtu kwa Mtu, na kwa pamoja, Argentina walikuwa bora, Wao
[Uswisi] wanatengeneza Saa nzuri sana lakini wana Wanasoka wachache.”
Huko Brazil, Argentina wameshinda Mechi
zao zote 4 hadi sasa na kufunga Bao 7 huku Messi akifunga Bao 4 kati ya
hizo lakini ushindi wote huo ulikuwa wa tofauti ya Bao 1 tu.
Katika Mechi zote hizo 4, Messi ndie alieibuka na Tuzo ya Mchezaji Bora wa kila Mechi.
Maradona aliongeza “Huyu Kijana [Messi]
yuko mpweke..Timu haibadilishi kasi yake, Mastraika hawazunguki. Nasikia
uchungu, hasira, fedheha, kwa sababu Argentina inaweza kucheza vizuri
zaidi, tena zaidi…Kocha lazima alazimishe hili! Kama hawataongeza ubora
dhidi ya Belgium, basi tuko mashakani! ”
Argentina wameshatwaa Kombe la Dunia
mara mbili na wakitwaa kwa mara ya 3, tena nyumbani kwa Mahasimu wao
Wakuu Brazil, hiyo itakuwa starehe kubwa kwa Mashabiki wa Argentina
ambao Maelfu yao wamefurika Brazil kushangilia Timu yao.
0 maoni:
Post a Comment