MAKAMANDA WA CHADEMA WANAOKABILIWA NA KESI YA UGAIDI WAREJESHWA RUMANDE-TABORA
Makamanda watano wa Chadema
wakiingizwa ukumbi wa mahakama ya hakimu mkazi mkoani Tabora
kufuatia kesi ya Ugaidi inayowakabili akiwemo kaimu Katibu wa Chama
hicho mkoa wa Dar-es-Salaam Bw.Henry Kileo aliyeshika Kitabu mkononi.
Wanachama watano wa chama cha Demokrasia na Maendeleo- CHADEMA
wanaokabiliwa na mashitaka ya Ugaidi wamerejeshwa tena rumande pasipo
maombi yao kusikilizwa hadi tarehe 22/07/2013 kesi hiyo itakapotajwa
tena.
Akitoa uamuzi huo hakimu mkazi mfawidhi wa mahakama ya mkoa wa
Tabora Issa Magoli amesema kuwa kwa vile mahakama yake haina uwezo
kisheria kusikiliza shauri hilo kesi hiyo inahairishwa hadi hapo upande
wa utetezi wakiendelea na taratibu za kupeleka hoja zao Mahakama
kuu.
Hakimu Magoli kabla ya kuahirisha shauri hilo aliwashauri mawakili wa
upande wa utetezi wawasilishe hoja zao mahakama kuu ya Tanzania ndipo
watakapoweza kupatiwa ufumbuzi wa kisheria.
Akizungumza nje ya Mahakama,Wakili wa washtakiwa hao,Peter
Kibatala,alisema wanafanya utaratibu wa kupeleka shauri lao Mahakama Kuu
baada ya kupewa nakala ya uamuzi uliotolewa na mahakama ya hakimu Mkazi
Tabora.
Alisema katika maombi yao Mahakama kuu wataomba ipitie shauri hilo na
pia kuona kama ni halali kisheria kwa washtakiwa hao kufunguliwa kesi
hiyo baada ya awali washtakiwa wanne ukimuondoa Kilewo mashtaka yao
kuondolewa na kasha kushtakiwa tena na Kilewo.
Wakili Kibatala mbali ya kusema ana imani na Mahakama lakini alieleza wana Imani zaidi na mahakama Kuu kwa vile alidai ipo huru
Alisisitiza kama mawakili wa washtakiwa wanapambana kuhakikisha haki
inatendeka na kuwaomba wana ndugu na jamaa kuwa watulivu na wawategemee.
“Nawaomba ndugu na jamaa wa washtakiwa kuwa watulivu wakituacha mawakili
wao tukipambana katika suala hili na tunawatia moyo msikate tama kwani
kesi ni suala la mchakato na linaweza kuchukua muda mrefu”Alisema
Kwa upande wake Mke wa mshtakiwa Henry Kilewo,Joyce Kiria,alisema yeye
alipoamua kuolewa na Kilewo alijua ni mwanaharakati lakini kwa vile
anampenda alikubali kuolewa naye.
Alisema yupo naye katika kipindi hiki na bado anampenda na kuwatia moyo
wanawake kuwa bega na waume zao pale wanapokuwa na matatizo.
“Nataka niwaambie kuwa hii sasa ndio wanawake live ni lazima wanawake
tuwe wavumilivu katika kupambana na tusibaki kulia lia”Alisema.
Shauri hilo lilivutia umati wa wapenzi wa CHADEMA waliojitokeza kwa
wingi huku ulinzi ukiwa mkali ambapo Askari wa kikosi cha kutuliza
Ghasia walitanda wakiwa na silaha.
Watuhumiwa hao watano akiwemo kaimu katibu wa Chadema Bw.Henry
Kilewo,Evodius Justian,Oscar Kaijage,Seif Kabuta na Rajabu Kihawa
wamerejeshwa rumande hadi hapo tarehe 22 Julai mwaka huu kesi hiyo
itakapotajwa tena.|Na KapipiJHabari
0 maoni:
Post a Comment