Majonzi hayo yaliongezeka zaidi Alhamisi baada ya Azam kuibuka na ushindi wa mabao 4-2 dhidi ya JKT Ruvu Uwanja wa Karume, Dar es Salaam, hivyo Azam kuipiku Yanga kileleni mwa msimamo ikiwa na pointi 22 ikiiacha Yanga nafasi ya pili na pointi zake 20.
Kutokana na hali hiyo, leo Yanga itashuka Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi Tabora kuivaa Kagera Sugar, ikiwa na dhamira moja ya kurejea kileleni mwa msimamo wa ligi hiyo. Kama Yanga ikishinda leo itafikisha pointi 23 na itaombea Azam FC ambayo kesho itacheza na Toto Africans Uwanja wa Azam Chamazi ipate matokeo mabovu.
Yanga inapewa nafasi ya kushinda leo kutokana na mwenendo mbaya wa wenyeji wao Kagera Sugar, ambao tangu kuanza msimu huu wameshinda mchezo mmoja na kupoteza mitano kati ya tisa waliyocheza.
Leo utakuwa mtihani wa pili kwa Kocha Mkuu wa Kagera Sugar, Mohammed Adolf Rishard, tangu akabidhiwe timu akirithi mikoba ya Mbwana Makatta aliyeachia ngazi kutokana na matokeo mabaya. Ni wazi Kocha Mkuu wa Yanga, Hans Pluijm naye ataingia uwanjani kuhakikisha vijana wake wanaibuka na ushindi ili kuwapa furaha mashabiki wao.
Hata hivyo pamoja na mwanzo mbaya wa Kagera Sugar, lakini timu hiyo inaweza kuzinduka na kufanya maajabu kwa kuifunga Yanga, kwani inakikosi bora cha wachezaji waliodumu kwa muda mrefu na timu hiyo akiwemo nahodha wake George Kavila na Paul Ngwai.
Yanga itaingia kwenye mchezo huo ikizidi kujivunia safu yake ya ushambuliaji inayoongozwa na Mzimbabwe, Donald Ngoma mwenye mabao saba na Amissi Tambwe ambao wamekuwa wakipambana kuhakikisha timu yao inafanya vizuri kwa kufunga mabao mengi.
Kwenye Uwanja wa Taifa Dar es Salaam, Simba inawakaribisha Majimaji ya Songea huku kocha wake Dylan Kerr, akijivunia ushindi wa bao 1-0, walioupata kwenye mchezo uliopita dhidi ya Coastal Union ya Tanga na timu hiyo kufikisha pointi 18 na kupanda hadi nafasi ya nne.
Mshambuliaji Hamisi Kiiza amekuwa tegemeo kwa kocha Kerr, katika upande wa mabao baada ya kufunga bao lake la sita Jumatano iliyopita ukiwa ni mchezo wake wa kwanza tangu kurejea uwanjani baada ya kukosa mechi tatu kutokana na kusumbuliwa na maumivu ya nyama za paja.
Pamoja na kuonesha kiwango cha chini kwenye mchezo uliopita, lakini Simba wanapewa nafasi ya kushinda mchezo wa leo kutokana na udhaifu wa wapinzani wao Majimaji waliopo nafasi ya 10 wakiwa na pointi 11.
Rekodi zinaonesha Majimaji imekuwa hatari msimu huu inapocheza nyumbani uwanja wa Majimaji Songea, lakini mambo huwa tofauti inapokuwa ugenini na takwimu zinaonesha imepoteza mchezo mmoja nyumbani na kushinda mitatu, huku ikifungwa michezo mitatu na miwili ikitoka sare.
Mechi nyingine za leo, Mtibwa Sugar inayoshika nafasi ya tatu kwenye msimamo, itakuwa nyumbani Uwanja wa Manungu kucheza na Mwadui FC ya Shinyanga na Prisons itakuwa nyumbani Uwanja wa Sokoine kuchuana na Ndanda FC ya Mtwara na Coastal Union itakuwa Uwanja wa Mkwakwani ikicheza na Mbeya City.