Wednesday, September 10, 2014


Na Baraka Mpenja, Dar es salaam
YANGA SC ina mpango wa kuweka kambi mjini Bagamoyo mkoani Pwani kujiandaa na mechi ya ngao ya Jamii kuashiria kuzinduliwa kwa msimu mpya wa ligi kuu soka Tanzania bara itayopigwa jumapili (septemba 14 mwaka huu) uwanja wa Taifa Dar es salaam.
Kiingilio cha chini katika mechi hiyo inayowakutanisha mabingwa na washindi wa pili wa msimu uliopita kitakuwa shilingi elfu 5 tu kwa viti vya kijani na bluu.
Viti vya rangi ya chungwa ni Tsh. 10,000, VIP C na B itakuwa 20,000/=, wakati VIP A ni Tsh. 30,000 na tiketi za elekroniki zitatumika katika mechi hiyo.
Msimu uliopita, Azam walitwaa taji wakati Yanga chini ya kocha Mholanzi, Hans van Der Pluijm walishika nafasi ya pili.
Uongozi wa Yanga umeamua kumchagulia eneo la Bagamoyo kocha Marcio Maximo ili kuwatuliza zaidi wachezaji wake.
Mara kadhaa msimu uliopita, Yanga walijichimbia Bagamoyo kujiandaa na mechi za ligi kuu na ligi ya mabingwa barani Afrika.
Wakati huo huo, Mabingwa wa ligi kuu Tanzania bara, Azam fc wanaendelea kujiandaa na mechi hiyo katika uwanja wao wa kisasa wa Azam Complex, uliopo Mbande , Chamazi, nje kidogo ya jiji la Dar es salaam.
Aggrey Maris aliyeikosa mechi ya kirafiki baina ya Taifa Stars na Burundi septemba 7 mwaka huu mjini Bujumbura kutokana na majeruhi, amerejea katika mazoezi hayo.
Lakini taarifa mbaya ni kwamba, nahodha wa klabu hiyo, John Bocco ‘Adebayor’ licha ya jana kufanya mazoezi katika Gym ya kisasa pale Chamazi-Azam Complex, vipimo alivyofanyiwa na mtaalamu (Physiotherapist), Gilbert Kigade katika Hospitali ya Msasani Peninsula vinaonesha kuwa nyota huyo mkali wa kufumania nyavu anatakiwa kukaa nje ya uwanja wa kwa wiki tatu.
Kwa maana hiyo, Bocco anayesumbuliwa na maumivu ya misuli ataikosa mechi ya jumapili dhidi ya Yanga na pia michezo mitatu ya ligi kuu soka Tanzania bara inayotarajia kuanza septemba 20 mwaka huu.

0 maoni:

Post a Comment

waliotembelea blog