Sunday, December 1, 2013

Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe amesema tuhuma alizosomewa na uongozi wa Chadema katika kikao cha Kamati Kuu sizo zilizoelezwa na chama hicho mbele ya waandishi wa habari na viongozi wa chama hicho.

Aidha, amesema kuwa vita aliyopo siyo kati ya Chadema na Zitto, bali ni vita ya watu wengi, akitaja magenge ya watu wanaotaka urais 2015 na walioficha fedha nje ya nchi walioungana wakiona tatizo lao ni yeye hivyo kutaka kumwondoa bungeni.

Akizungumza katika mahojiano maalumu na gazeti hili kwa njia ya simu, Zitto alisema kuwa hadi sasa bado hajapokea tuhuma 11 anazokabiliwa nazo, hivyo hajui makosa hayo na bado anasubiri akabidhiwe kwa maandishi.

Ana ugomvi gani na viongozi wenzake?

Alipotakiwa kueleza iwapo ana ugomvi na watu ndani ya Chadema, Zitto alisema kuwa huenda mambo hayo yanatokea kwa sababu mahasimu wake wa kisiasa wa ndani na nje wameamua kuungana na kupambana naye ili kumdhoofisha kisiasa kwa masilahi yao.

“Matatizo yaliyopo ni mafanikio yangu, …. nadhani hii siyo vita kati ya Chadema na Zitto, bali ni vita ya watu wengi, pengine magenge ya watu wanaotaka urais na wale walioficha fedha zao nje wamekaa pamoja wanaona tatizo lao ni Zitto… wanajua siwezi kusemea nje maana sina kinga…, hivyo wanataka kuniondoa bungeni…” alisema.

Aliongeza kuwa kwenye siasa kinachohitajika ni kusimamia misingi, jambo alilosema binafsi amekuwa akilifanya katika kipindi chake chote cha kisiasa.

Zitto alisema kuwa ni vyema wananchi wakawapima wabunge wao kwa kazi wanazozifanya bungeni akibainisha kuwa kati ya mwaka 2011 hadi 2013, yeye amewasilisha hoja nyingi nzuri zilizo na mashiko ikilinganishwa na wabunge wenzake wanaomtuhumu kutumiwa na CCM.

“Je, mbunge anayetumika na Chama Cha Mapinduzi anaweza kupeleka hoja ya kumng’oa Waziri Mkuu na kumshinikiza Rais mpaka akasimamisha kazi mawaziri wanane? Je, mbunge anayetumika anaweza kushikia bango watu wanaotorosha fedha nje ya nchi?” alihoji Zitto.

Tuhuma za usaliti

“Sizijui hizo tuhuma 11 kwa sababu nilichoelezwa kwenye kikao cha Kamati Kuu sicho kilichoelezwa na chama kwenye mkutano wake na waandishi wa habari… hivyo sijui kabisa hizo tuhuma zangu ni zipi mpaka sasa,” alisema.

Alisema kuwa kwenye Kamati Kuu alilaumiwa kwa masuala matatu. Akizitaja: “Nililaumiwa kuwa sifanyi kazi za chama, la pili kuwa nimemwagiza Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali akague vyama kutokana na kuwa na nia mbaya na chama hicho. Tuhuma ya tatu ni ile ya kukataa kupokea posho bungeni ambapo nadaiwa kulenga kuwadhalilisha wabunge wenzangu.”

0 maoni:

Post a Comment

waliotembelea blog