Sunday, November 17, 2013

KAMA utahitajika kuwataja wasanii kumi wanaofanya vizuri katika muziki wa Injili Bongo na hata Afrika Mashariki, haitakuwa rahisi kuyaacha majina ya Rose Mhando, Bahati Bukuku, Upendo Nkone, Upendo Kilahiro, Christina Shusho, Siana Ulomi, Martha Mwaipaja, Jeni Miso na Jennifer Mgendi.

Ni kwasababu hao ni waimbaji ambao katika kila duka linalouza kazi za muziki huo, ni vugumu kupita saa mbili kabla mmoja wao hajauza kazi yake.

Katika wakati ambao wanamuziki wa Bongo Flava na dansi wanalilia kupata soko la kazi zao, waimbaji wa Injili wanaendelea kula kuku kwa mrija kwani kazi zao sokoni zinanunuliwa kama njugu.

Kwa baadhi ya nchi, nyimbo zao hupigwa hata katika kumbi za starehe kwa kuamini ni nyimbo za kujirusha kutokana na mvuto wake.

Rose Mhando

Huyu ndiye kiboko yao, wanamuziki wa Bongo Flava wanamfahamu kwa jinsi anavyowapiga bao katika uuzaji wa kazi zake, si tu katika CD na video, Rose Mhando pia ni kinara wa mauzo katika miito ya simu.

Diamond ambaye anasifika kwa kuuza miito ya simu, akikutana na Rose Mhando anakaa chini kwani mapema mwaka huu alimwacha mbali kwa kuingiza Sh29 milioni ndani ya miezi mitatu huku Diamond akiingiza Sh21 milioni.

Albamu zake za ‘Mteule Uwe Macho’, ‘Kitimutimu’, ‘Jipange Sawasawa’ na ‘Utamu wa Yesu’ bado zinaendelea kufanya vizuri pamoja na kuwa wasanii wengine wanaingiza albamu mpya kila kukicha.

Bahati Bukuku

Huyu anatajwa kushikilia nafasi ya pili ya mauzo ya CD na video katika maduka mbalimbali ya kazi za sanaa Bongo. Pamoja na kutotoa kazi mpya mara kwa mara, albamu yake moja ilimfanya kuwa mwimbaji namba mbili katika mauzo na matamasha nchini.

Tamasha lolote la Injili haliwezi kukamilika bila kupigwa nyimbo kama ‘Waraka wa Amani’, ‘Nimesamehewa Dhambi’, ‘Nyakati za Mwisho’ na ‘Mapito’.

Mwanamuziki huyu kwa sasa anatamba na albamu mpya aliyoizindua mwezi uliopita iitwayo ‘Dunia Haina Huruma’.

Upendo Kilahiro

Inavyoonekana muziki wa Injili unamlipa sana kwani ameweza kuanzisha Chuo cha Ushonaji kiitwacho, New Day Africa Foundation, ambacho wanafunzi wake hawalipi hata shilingi moja kwa muda wanaochukua ujuzi chuoni hapo.

Kilahiro anayetamba na nyimbo za ‘Unajibu Maombi’ na ‘Usinipite’, ni msanii namba tatu kwa mauzo ya nyimbo za Injili Bongo.

Upendo Nkone

‘Niacheni Niimbe’, ‘Nimebaki na Yesu’, ‘Uniongoze Yesu’ na ‘Nakaza Mwendo’, ni baadhi ya nyimbo zinazofanya kazi zake ziendelee kununuliwa kwa wingi. Kila anapoachia wimbo mpya, huendelea kuzifanya zile za zamani ziwe nzuri zaidi.

Mbali na kuuza kazi zake, pia ni mwanamuziki anayeongoza kwa kufanya matamasha ndani na nje ya Bongo. Mara kwa mara hufanya ziara nchini Kenya ambako anakubalika na kuheshimika.

Christina Shusho

Huyu anazo sababu zaidi ya mia moja za kuwa mwanamuziki anayeuza sana katika muziki wa Injili. Kwanza sura yake inapokaa kwenye ‘kava’ inampa mteja hamu ya kutoa pesa yake kununua CD, pili unapopata bahati ya kuisikia sauti yake kwa mara ya kwanza, hakika utataka kuisikia tena na tena na tatu tungo zake zinazogusa maisha ya kawaida na kiroho zimekuwa kivutio kikubwa.

Flora Mbasha, Jeni Misso, Jennifer Mgendi, Martha Mwaipaja na Siana Olomi nao wanaingia kwenye kundi hilo, lakini wanapishana kidogo kutokana na sababu mbalimbali zilizotolewa na wafanyabiashara wa kazi hizi.

Waimbaji Jeni Misso, Martha Mwaipaja na Siana Olomi ni kama wanachipukia kwenye soko kuu la kazi hizi, lakini wamekuwa wakichuana na wakongwe akina Flora Mbasha na Jennifer Mgendi ambao wamekuwa katika muziki huu kwa muda mrefu.

Wafanyabiashara wa kazi hizi wanasema, Jennifer Mgendi na Flora Mbasha, waliwahi kuwa vinara wa mauzo lakini walipoanza kujichanganya na biashara nyingine iliwapunguzia mashabiki ambao walianza kununua kazi za waimbaji wengine.

Flora Mbasha kujihusisha na kampeni mbalimbali zikiwamo za  vyama vya siasa na Jennifer Mgendi kujiingiza katika uigizaji wa filamu, zinatajwa kuwa ni sababu zilizowarudisha nyuma.

Yote kwa yote hii ndiyo ‘krimu’ ya wasanii wanaoongoza sokoni kwa muziki huo, tamasha lolote la muziki wa Injili Bongo au Afrika Mashariki, haliwezi kukamilika

0 maoni:

Post a Comment

waliotembelea blog