MTALII
mmoja raia wa Marekani, Thomas Macfee (58), ameuawa na kundi la tembo
wakati akiwa kwenye kambi ya Kakoi Tarangire eneo linalodaiwa kuwa ni
mapito ya asili ya wanyama hao.Kaimu
Kamanda wa Polisi mkoani Manyara, Musa Marambo, alisema kuwa tukio hilo
lilitokea Agosti 30 mwaka huu, saa 2:30 asubuhi baada ya mtalii huyo
akiwa na wenzake watano ambao majina yao hayakupatikana kujaribu kupiga
picha za kundi kubwa la tembo lililokuwa likipita karibu na eneo
walilokuwa.Alisema
kuwa wakiwa kwenye harakati za kupiga picha, ghafla tembo hao
walibadili uelekeo na kuanza kuwafuata ndipo wakaanza kukimbia ambapo
kwa bahati mbaya Macfee alinasa kwenye dimbwi la matope.
“Baada ya kunasa kwenye matope
alishindwa kutoka ndipo tembo wale wakaanza kumpitia juu na baada ya
hapo wenzake walienda kumchukua na kumuwahisha kwenye zahanati ya
hifadhi ya taifa ya Tarangire ndipo akafariki,” alisema Manyara.
Alisema
kuwa baada ya kufariki alipelekwa kuhifadhiwa kwenye hospitali ya Selian
jijini Arusha ambapo ubalozi wa Marekani ulimchukua kwa ajili ya
taratibu za mazishi.
Meneja
uhusiano wa Tanapa, Paschal Shelutete, alitoa taarifa kwa vyombo
mbalimbali vya habari akifafanua kuwa eneo alilokuwa mgeni huyo ni nje
ya hifadhi yao.
“Tukio la
mgeni husika lilitokea nje ya hifadhi ya Tarangire katika kijiji cha
Kakoi kambi ya Tarangire River Camp, wakiwa wanafanya utalii wa kutembea
kwa miguu.”
“Baada ya
kuvamiwa na kuumizwa, mgeni huyu alifikishwa katika zahanati ya
Tarangire na watumishi wa kambi aliyofikia ambayo iko nje ya hifadhi kwa
ajili ya matibabu ya huduma ya kwanza ambapo alifariki,” alisema.
0 maoni:
Post a Comment