MJADALA wa Bunge jana jioni ulitawaliwa na kauli nzito baada ya
wabunge kadhaa wa Chama cha Mapinduzi (CCM), kutuhumiana kuhusika na
ubadhirifu katika vyama vya ushirika nchini.
Hoja hiyo iliibuka wakati Bunge likijadili muswada wa sheria ya vyama
vya ushirika wa mwaka 2013 uliowasilishwa na Waziri wa Kilimo, Chakula
na Ushirika, Balozi Christopher Chiza.
Aliyekuwa wa kwanza kuwasha moto huo baada ya mapumziko ya mchana
alikuwa mbunge wa Busega, Dk.Titus Kamati (CCM), ambaye alisema waziwazi
kuwa wanasiasa ndio wezi wa vyama vya ushirika.
Dk. Kamani alihoji ni kwa nini serikali inapata kigugumizi
kuwachukulia hatua wahusika na kusisitiza kuwa hapo kuna kulegalega
kumaliza ufisadi katika ushirika.
“Wanasiasa hawa kwa nafasi zao wameingia kwenye ushirika na kufanya ufisadi lakini serikali inashindwa kuwachukulia hatua.
“Huku ni kulegalega na ndio maana hata tumeshindwa kuwataja wauza dawa
za kulevya, waziri anaishia kusema tunayo orodha,” alisema.
Alihoji ni kwa nini sasa serikali isiige mfano wa China wa kuwafunga
na hata ikibidi kuwanyonga watuhumiwa wa ufisadi wa vyama hivyo
ikithibitika bila kujali nafasi zao kwenye siasa.
Mbunge wa Mpanda Vijijini, Moshi Kakoso (CCM), ndiye aliyefuata na
kuchafua hali ya hewa kwa kumtuhumu Mkurugenzi wa Bodi ya Tumbaku Nchini
(TTB) kufanya ufisadi mkubwa ambao serikali inaujua lakini imeamua
kuunyamazia.
Bila kumtaja kwa jina lakini alikuwa akimlenga mbunge mwenzake wa
Namtumbo, Vita Kawawa, akisema kuwa anajilipa mshahara mara mbili ya ule
uliopitishwa na serikali.
Alisema kuwa analipwa sh milioni mbili za mawasiliano na anachukua
dola 1200 (zaidi ya sh milioni 1.8) kwa ajili nyumba badala ya sh
800,000 zilizoidhinishwa.
Mbunge huyo alisema mwenyekiti huyo anayajua mambo hayo na ndiye aliyeidhinisha.
“Nina uhakika na ninachozungumza, waziri nilishamletea taarifa juu ya
jambo hili lakini amenyamaza, hivi hapa tunategemea ushirika utakuwa hai
wakati mabosi wanautafuna?” alihoji.
Wakati mbunge huyo anaendelea kuzungumza, Kawawa akitaka kumpa taarifa juu ya jambo analolizungumza.
Kawawa alisema muda wake wa kuwa mwenyekiti kwenye bodi hiyo uliisha
Juni 31 mwaka huu, hivyo ni vema mbunge mwenzake akatoa ushahidi wake
juu ya tuhuma za watendaji wa bodi husika.
Baada ya Kawawa kumaliza, Kakosa aliendelea kuchangia ambapo alikataa
taarifa hiyo kwa madai ana ushahidi wa kile kilichofanyika.
Mara baada ya Kakoso kumaliza kuchangia muswada huo, mbunge wa Kondoa
Juma Nkamia alipewa fursa ya kutoa taarifa ambapo alisema tuhuma
zilizotolewa na Kakoso dhidi ya Kawawa ni nzito sana na Bunge lipate
fursa ya kuangalia jambo hilo pamoja na mhusika kutoa ushahidi.
Naibu Spika, Job Ndugai, alisema ofisi ya Bunge iko wazi kwa Kakoso kuwasilisha ushahidi wake juu ya kile alichosema.
Mara baada ya Ndugai kutoa ufafanuzi huo, alimpa nafasi mbunge wa
Sikonge, Saidi Nkumba (CCM), ambaye alimtuhumu Kakoso kwa kushindwa
kuliambia ukweli Bunge kuwa yeye ni Mwenyekiti wa Chama Kilele (APEX)
ambacho kinapigiwa kelele kuwa kinawanyonya wakulima.
Alisema wakiwa Dar es Salaam kwenye vikao vya kamati za Bunge, Katibu
wa Apex, aliitwa katika kamati kama mdau ambapo alipobanwa juu ya wizi
unaofanyika kwenye chombo hicho alisema serikalini ikiiba kelele
zinapigwa lakini APEX ikiiba kidogo kelele zinakuwa kubwa sana.
“Katibu wa Kakoso ndiye aliyetuambia hivyo. Huu ni wizi, sisi hatuwezi
kukubaliana na jambo hilo, serikali haivumilii wizi, huyu Kakoso
anasema APEX ni mkombozi lakini pale Tabora wamewaibia wananchi bilioni
16, hivi kweli hizi si fedha nyingi?
“Hii APEX ni lazima ifutwe, wenye tamaa ya kwenda kwenye ushirika ni
vema waache siasa, na wenye ushirika ni vema wakabaki huko huko.”
Alibainisha kuwa wizi unaofanyika kwenye vyama vya ushirika
unasababishwa na wanasiasa ambao wana kinga za kisiasa ndiyo maana
wanaendelea kutafuna fedha za wananchi.
Mbunge wa Kasulu Mjini, Moses Machali, alisema wabunge wana taarifa za
wizi wanatoa taarifa hapa bungeni lakini hakuna wanachokifanya.
“Yaani kila kukicha mnalea wizi halafu leo hii mnaanzisha tume za
kuwanyonya wakulima, kule kwangu wakulima waliuza tumbaku, msianzishe
vitu vya ajabu ajabu…, huu ni wizi mtu, msituletee wizi hapa kwa
kubadilisha majina ya vitu,” alisema.
Tundu Lissu wa Singida Mashariki (CHADEMA) alisema
sababu kubwa ya kuporomoka kwa ushirika ni serikali kuuingilia, kuudhibiti na kuuporomosha.
Alisema serikali ilianza kuvuruga mambo 1966 sheria za ushirika
ilibadilishwa na msajili wa vyama vya ushirika alipewa mamlaka ambayo
alianza kuyatumia vibaya ambapo mwaka 1976 alipigwa marufuku zikaja bodi
za mazao.
Mwaka 1982 vilirejeshwa vyama vya ushirika lakini mamlaka yake yalikuwa yakitolewa na mrajis ambaye ni serikali.
Mbunge wa Nzenga, Andrew Kigwangalah, aliibua upya mzozo wa awali kwa
kuanika nyaraka za ufisadi katika TTB kama ilivyokuwa imedokezwa awali
na Kakoso.
Kingwangalah ambaye alidai kuwa hatarudi nyuma kuwataja mafisadi na
wauza dawa za kulevya alisema kuwa kodi ya nyumba ya mwenyekiti wa bodi
inalipiwa gahara tofauti na ile iliyoidhinishwa.
Alionyesha nyaraka kadhaa za malipo ya viongozi wa bodi hiyo na kisha
kumvaa Nkumba akisema kuwa tatatizo la nchi hii si Apex bali ni rushwa,
wizi, ubadhirifu halafu watu wanaona wizi wanaungalia badala ya kuchukua
hatua.
“Waliobaki kwenye ushirika ni wezi watupu, wazalendo wameisha, wezi tunawajua lakini hatuwawajibishi wala kuwachukulia hatua.
“Nkumba ni msaidizi wa Kawawa katika bodi ya tumbaku anajua ukaguzi
haujafanyika na ukifanyika wao hawatasalimika ndiyo maana wanaanza
kuipiga vita Apex.
“Kuna watu wanatumiwa na kampuni za ubebari ambazo zilikuwa
zikisafirisha tumbaku na kusambaza pembejeo, hawa sasa wanaona hatari za
kampuni zao ndiyo maana zinawatumia wabunge ili APEX ifutwe, tuwe
makini na wabunge waovu,” alisema.
Mzozo huo ulidumu huku Kawawa na Nkumba wakisimama kujitetea bila
mafanikio hatua iliyomlazimu Naibu Spika wa Bunge kutoa nafasi kwa
baadhi ya wabunge kuomba viongozi, lakini akaliahirisha Bunge hadi leo
ambapo atatoa uamuzi wake.
Mapema asubuhi, wabunge walipendekeza wabadhirifu wa mali za ushirika
walazimishwe kufidia hasara iliyotokea pamoja na kufilisiwa mali zao.
Pendekezo hilo limetolewa na Nkumba alipokuwa akisoma hotuba ya
Mwenyekiti wa
Kamati ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji, Peter Msolla.
Nkumba alisema ushirika umewakatisha tamaa wananchi kutokana na
ubadhirifu wa viongozi wake hivyo ujio wa sheria hiyo utakuwa mkombozi.
Aliongeza kuwa watuhumiwa wa ubadhirifu wa ushirika wafikishwapo
mahakamani mashauri yake yamekuwa hayathibitiki licha ya taarifa za
fedha kuonyesha kuwa upotevu fedha upo; ni vema kuwepo na utaratibu wa
kuwabana wahusika.
Nkumba alisema vyama vya ushirika vimekuwa vikikaguliwa na Shirika la
Ukaguzi na Usimamizi wa Vyama vya Ushirika (Coasco) ambalo halifanyi
kazi zake vizuri na kuitaka serikali kuweka utaratibu mzuri ikiwemo
kuhusishwa kwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za serikali.
Waziri wa Kilimo, Chiza alisema kuundwa kwa sheria hiyo litakuwa suluhisho la matatizo ya ushirika nchini.
Alisema serikali inalenga kuifuta sheria ya vyama vya ushirika namba
20 ya mwaka 2003 na inaamini sheria mpya itaimarisha, kuendeleza na
kuufufua ushirika.
Chiza alisema sheria ya ushirika ya mwaka 2013 ina lengo la kutekeleza
sera ya maendeleo ya ushirika ya mwaka 2002, inayovitaka vyama vya
ushirika imara, endelevu na vyenye kukidhi mahitaji ya wanachama
kiuchumi chini ya mazingira ya soko huria.
0 maoni:
Post a Comment