Wednesday, August 7, 2013


Katibu mkuu wa Baraza la wazee Ibrahim Akilimali (katikati) akiongea na waandishi wa habari le makao makuu ya klabu, kushoto kwake ni mzee Bilal Chakupewa na kulia kwake ni mzee Jabir Katundu
Uongozi wa klabu ya Young Africans umetangaza mkutano mkuu wa dharura wa wanachama wote utakaofanyika tarehe 18.08.2013 katika ukumbi wa PTA sabasaba eneo la mtoni jijini Dar es salaam.
Akiongea na waandishi wa habari leo makao makuu ya klabu hiyo, katibu mkuu wa Yanga Lawrence Mwalusako amesema mwenyekiti wa klabu ameamua kuitisha mkutano mkuu huo wa dharula  kwa ajili ya kupata maoni ya wanachama juu ya mustakabali wa TPL kuingia makubaliano na TV ya Azam kuonyesha michezo ya Ligi Kuu.
Mwalusako amesema kwa mfumo wa klabu ya Yanga, wanachama ndio wana maamuzi ya mwisho juu ya mustakabali wa timu yao kuhusiana na masuala ya klabu yao, hivyo tumeona ni bora kurirudisha suala hili kwa wanachama ili waweze kutoa mchango wao.
Katibu wa baraza la wazee wa klabu ya Yanga mzee Ibrahim Akilimali akiongea kwa niaba ya wazee wa klab hyo, amesema wao wanaungana na kamati ya utendaji  juu ya msimamo wao wa kutotaka Azam Tv kurusha michezo yake yote watakayocheza.
Sisi wazee wa Yanga tunaunagana na mwenyekiti, Kamati Kuu ya Utendaji na viongozi wa matawi kuwa hatupo tayari kuona kampuni ya Azam Media kupitia kupitia kituo chake cha Azam TV inaonyesha mchezo wetu wowote wa Ligi Kuu.
Ifuatayo ni  Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari,
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI.
1. Hivi karibuni tumepata uhakika kuwa Tanzania Premier League (TPL) na Azam Media wanayo nia ya kuingia mkataba wa kuonyesha mechi za Ligi Kuu (Premier League) kwa msimu wa 2013/2014, 2014/2015 na 2015/2016
2. Baada ya Kamati ya Utendaji ya YANGA kufanya uchambuzi wa kina juu ya taarifa ya makubaliano ya kibiashara ya TPL / Azam Media ilihitimisha kuwa mkataba huu hauna maslahi kwa YANGA, na kwa hivyo Kamati ya Utendaji ya YANGA ilifikia uamuzi kuwa mechi za YANGA zisirushwe hewani na Azam Media.
Kwa kuwa wawazi, Kamati ya Utendaji ya YANGA ilitoa taarifa kwa wanachama wa YANGA kupitia vyombo vya habari tarehe 29 Julai, 2013 ambapo iliweka bayana sababu zake na kueleza kuwa YANGA haina tatizo na vilabu vingine vya mpira wa miguu ikiruhusu mechi zao kurushwa na Azam Television ila haifurahii kuwa TPL inalazimisha YANGA kuonyesha mechi zake za Vodacom Premier League katika Azam Television.
3. Sote tumeona baada ya hapo kuwa “nguvu ya ziada” inatumika kupotosha msimamo wa Kamati ya Utendaji ya YANGA na kuidhalilisha Klabu ya YANGA hadharani.
Juu ya hayo na kwa kushangaza sana, baadhi ya vilabu vya mpira wa miguu ambavyo vina sifa kuwa havijawahi kushinda Ligi Kuu, vimeundwa hivi juzi tu, havina uzoefu wowote wa kucheza soka kimataifa n.k. vina kuja kuyapinga Kamati ya Utendaji ya YANGA jinsi ya kuendesha shughuli za klabu ya Yanga, vikiwa vinasahau vilabu vyao wenyewe na badala yake kuiingilia YANGA kwa sababu zinazojionyesha wazi.
Inadhihirika wazi kwamba kuna ushirikiano usio mzuri unaoashiria kula njama kuilazimisha YANGA iruhusu mechi zake zirushwe na Azam Television.
Kwa kuwa YANGA ni Klabu ya Wanachama yenye kupata nguvu kutokana na misingi yake ya kidemokrasia iliyojijengea na uamuzi wake wa mwisho unatokana na Wanachama wake mwenyewe, umeamua kuliweka suala hili zima kwa Wanachama wa Yanga ili waamue ni njia gani ya kufuata kwa maslahi ya Klabu yetu.
Kwa kuzingatia hali hiyo basi, na kulingana na mamlaka niliyonayo kama Mwenyekiti wa YANGA, natangaza mkutano wa dharura wa Wanachama wa YANGA tarehe 18 Agosti, 2013 utakaofanyika uwanja wa Sabasaba kwenye ukumbi wa PTA saa 3.30 asubuhi waje tujadiliane na kuamua suala la Azam Television kurusha mechi za YANGA.

0 maoni:

Post a Comment

waliotembelea blog