LIGI DARAJA LA KWANZA
Mechi namba 34 (Pamba vs Friends Rangers). Kamishna wa mechi hiyo
Mnenge Suluja amepewa Onyo Kali kwa kutoripoti kitendo cha timu ya Pamba
kuhudhuria kikao cha maandalizi ya mechi (pre match meeting) ikiwa na
wawakilishi watatu badala ya wanne. Kitendo hicho ni kinyume na Kanuni
ya 14(2b) ya Ligi Daraja la Kwanza.
Mechi namba 35 (Kiluvya United
vs Lipuli). Timu ya Lipuli imepewa Onyo Kali kwa kuhudhuria kikao cha
maandalizi ya mechi (pre match meeting) ikiwa na wawakilishi watatu
badala ya wanne. Kitendo hicho ni kinyume na Kanuni ya 14(2b) ya Ligi
Daraja la Kwanza.
Pia mshabiki wa Kiluvya United, Bw. Athuman
Mzongela anapelekwa Kamati ya Nidhamu kwa kuwavamia waamuzi na kutaka
kuwapiga wakati wa mapumziko. Hata baada ya mchezo aliendelea kuwatolea
lugha chafu waamuzi na Msimamizi wa Kituo.
Mechi namba 36 (African
Sports vs Ashanti United). Daktari wa Ashanti United, Andrea Mbuguni
amefungiwa miezi sita na kupigwa faini ya sh. 200,000 kwa kuondolewa
kwenye benchi baada ya kumtolea lugha chafu Mwamuzi Msaidizi namba moja.
Mechi namba 38 (Lipuli vs Mshikamano FC). Kocha wa Mshikamano FC,
Hamisi Kinonda amefungiwa mechi tatu na kupigwa faini ya sh. 300,000
baada ya kuondolewa kwenye benchi kwa kupinga muda wa nyongeza wa dakika
tano, na kumtolea lugha ya matusi Mwamuzi wa Akiba. Adhabu hiyo ni kwa
mujibu wa Kanuni ya 40(11) ya Ligi Daraja la Kwanza.
Wachezaji wa
Mshikamano FC, John Mbise jezi namba 9, Abdallah Makuburi (5), Ally
Mangosongo (12) na kipa Steven Peter (1) wanapelekwa Kamati ya Nidhamu
ya TFF kwa kumshambulia Mwamuzi Bryson A. Msuya.
Lakini pia Mwamuzi
Bryson A. Msuya amefungiwa mwaka mmoja kwa kutozingatia sheria ipasavyo
wakati akitoa penalti dhidi ya timu ya Mshikamano FC, na ripoti yake
kufanana na ile ya Kamishna.
Mwamuzi Msaidizi Namba Moja, Makongo
Katuma amefutwa katika orodha ya waamuzi wanaotambuliwa na TFF kwa
kuwapiga vichwa wachezaji wawili wa Mshikamano FC wakati Mwamuzi wa Kati
alipokuwa akishambuliwa na wachezaji wa timu hiyo wakati wakipinga
adhabu ya penalti dhidi yao.
Adhabu hizo ni kwa mujibu wa Kanuni ya
38(1) na 38(1c) na (1e) za Ligi Daraja la Kwanza kuhusu Udhibiti wa
Waamuzi. Mwamuzi Katuma pia alipata alama za chini ambazo zisingemruhusu
kuendelea kuchezesha Ligi Daraja la Kwanza.
Naye Mwamuzi wa Akiba,
Hashim Mgimba ameondolewa kwenye ratiba kwa kuonyesha muda wa nyongeza
(added time) tofauti na ule alioelekezwa na Mwamuzi. Adhabu dhidi ya
Mgimba imezingatia Kanuni ya 38(1d) ya Ligi Daraja la Kwanza.
Kamishna wa mechi hiyo Fidelis Ndenga wa Njombe ameondolewa kwenye
ratiba ya makamishna kwa taarifa yake kufanana na ile ya Mwamuzi. Adhabu
hiyo imetolewa kwa kuzingatia Kanuni ya 39(1) ya Ligi Daraja la Kwanza
kuhusu Udhibiti wa Makamishna.
Pia Kamati imetoa mwito kwa vyombo
vya usalama (askari polisi) kutumia nguvu za wastani katika kutuliza
ghasia viwanjani, hasa pale wanapotaka kushughulikia eneo linalohusu
wachezaji.
Uwanja wa Kichangani umeondolewa kutumika kwa mechi za
Ligi, hivyo klabu za Iringa sasa timu zao zitatumia Uwanja wa Kumbukumbu
ya Samora mjini humo kwa mechi zao la Ligi. Uwanja huo ulikuwa kwenye
matengenezo ambayo tayari yamekamilika.
Mechi namba 39 (Polisi Dar
vs Pamba FC). Klabu ya Pamba imepewa Onyo Kali kwa kutofika kwenye kikao
cha maandalizi ya mechi (pre match meeting). Adhabu hiyo ni kwa mujibu
wa Kanuni ya 14(3) ya Ligi Daraja la Kwanza.
Mechi namba 33 (KMC vs
JKT Mlale). Kocha wa JKT Mlale, Edgar Msabila amefungiwa mechi tatu na
kupigwa faini ya sh. 300,000 baada ya kuondolewa kwenye benchi la ufundi
(orderd off) kwa kutoa lugha chafu. Adhabu hiyo ni kwa mujibu wa Kanuni
ya 40(11) ya Ligi Daraja la Kwanza.
Mechi namba 38 (Kimondo FC vs
Njombe Mji). Kocha wa Njombe Mji, Abdul Banyai amefungiwa mechi tatu na
kupigwa faini ya sh. 300,000 kwa kumtolea Mwamuzi lugha ya matusi, na
kulazimisha wachezaji wake wajiangushe ili kupoteza muda.
Mechi
namba 40 (Coastal Union vs Kurugenzi). Wachezaji wawili wa Kurugenzi;
Kipa Hamza Mpatula na Optatus Lupekenya wamefungiwa mechi tatu na
kupigwa faini ya sh. 300,000 kila mmoja kwa kosa la kupigana wakiwa
uwanjani baada ya mechi kumalizika. Adhabu hiyo ni uzingativu wa Kanuni
ya 37(3) ya Ligi Daraja la Kwanza kuhusu Udhibiti wa Wachezaji.
Mechi namba 36 (Rhino Rangers vs Polisi Mara). Klabu ya Rhino Rangers
imepigwa faini ya sh. 300,000 kwa kuchelewa kufika uwanjani kwa dakika
20. Adhabu hiyo imezingatia Kanuni ya 14(9) ya Ligi Daraja la Kwanza.
Mechi namba 38 (Mgambo Shooting vs Rhino Rangers FC). Kocha wa Mgambo,
Moka Shabani amefungiwa mechi tatu na kupigwa faini ya sh. 300,000 kwa
kutoa lugha ya matusi kwa Mwamuzi wakati timu zikielekea vyumbani baada
ya kumalizika kipindi cha kwanza. Adhabu hiyo ni kwa mujibu wa Kanuni ya
40(1) ya Ligi Daraja la Kwanza.
LIGI DARAJA LA PILI
Mechi namba 17 (Abajalo vs Burkina Faso). Klabu ya Burkina Faso
imepigwa faini ya sh. 100,000 kwa kutohudhuria kikao cha maandalizi ya
mechi (pre match meeting). Adhabu imezingatia Kanuni ya 14(3) ya Ligi
Daraja la Pili kuhusu Taratibu za Mchezo.
Mechi namba 18
(Cosmopolitan vs Changanyikeni). Klabu ya Changanyikeni FC imepigwa
faini ya sh. 200,000 kutokana na washabiki wake kuingia uwanjani
kushangilia ushindi baada ya filimbi ya mwisho. Adhabu hiyo ni kwa
mujibu wa Kanuni ya 42(1) ya Ligi Daraja la Pili kuhusu Udhibiti wa
Klabu.
Mechi namba 19 (Kariakoo vs Cosmopolitan). Klabu ya Kariakoo
imepewa Onyo Kali kwa timu yake kutokuwa na daktari katika mechi hiyo.
Adhabu hiyo imezingatia Kanuni ya 14(3).
Mechi namba 16 (Sabasaba
vs Namungo). Klabu ya Sabasaba imepewa Onyo Kali kutokana na washabiki
wake kuwazonga waamuzi wakati wakielekea vyumbani baada ya mechi hiyo
iliyochezwa Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro kumalizika. Uamuzi huo
umezingatia Kanuni ya 42(1) ya Ligi Daraja la Pili.
Mechi namba 17
(Mawezi Market vs Mkamba Rangers). Mkamba Rangers imepigwa faini ya sh.
100,000 kwa kutohudhuria kikao cha maandalizi ya mechi (pre match
meeting), na pia kuchelewa kufika uwanjani kwa dakika 35. Adhabu hiyo
imezingatia Kanuni ya 14(3) ya Ligi Daraja la Pili.
Mechi namba 19
(Namungo vs Mighty Elephant). Mighty Elephant imepigwa faini ya sh.
100,000 kutokana na wachezaji wa akiba na viongozi wake kuingia uwanjani
kushangilia bao la timu yao. Kitendo hicho ni kinyume na Kanuni ya
14(7), na adhabu hiyo ni kwa mujibu wa Kanuni ya 14(47) ya Ligi Daraja
la Pili.